Mwenyekiti wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania (VIWAWA), Leonard Mapolu, amewahimiza vijana nchini kuthamini na kulinda amani iliyopo pamoja na kuuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Mapolu amesema kuwa muungano huo ni alama ya
mshikamano wa Watanzania na unapaswa kulindwa kwa nguvu zote, kwani umekuwa
chachu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameonya kuwa jitihada zozote za kuvuruga amani
zinapaswa kupuuzwa na kukemewa kwa pamoja kwani wanaofanya hivyo hawana nia
njema na wanapaswa kupuuzwa.
Akizungumzia suala la amani, Mapolu alieleza
kuwa amani inaanza kwa mtu binafsi katika maisha ya kila siku, hususan katika
utoaji wa huduma. Alisisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kutenda haki kwa
wengine ili kuhakikisha mazingira ya utulivu yanaendelea kudumishwa katika
jamii.
Aidha, amesema kuwa uzoefu wake wa kuzunguka
maeneo mbalimbali ya nchi katika shughuli za utume umemuwezesha kuona namna
ambavyo amani ilivyo muhimu katika kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Ameeleza kuwa bila amani isingekuwa rahisi kufika na kuhudumia jamii katika
maeneo mbalimbali.
Mapolu amewasihi vijana kutambua nafasi yao
kubwa katika kulinda amani ya nchi, akisema kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa na
wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha utulivu unaendelea kudumu.
Amewatahadharisha vijana dhidi ya kutumika vibaya na watu wenye nia ya kuvuruga
amani.
Kwa upande mwingine, amesisitiza umuhimu wa
vijana kujenga mshikamano, kuheshimiana na kushiriki katika shughuli za
maendeleo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa
jamii. Ameeleza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji utulivu na ushirikiano wa
wananchi wote pamoja na maridhiano.
Akihitimisha, Mapolu ametoa wito kwa vijana
na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote,
akibainisha kuwa amani ni tunu adhimu inayopaswa kuhifadhiwa kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kijacho.
