
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA wakitoka mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili wanachama 17 wa chama hicho.
Wanachama 17 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kupanga kufanya matendo ya kigaidi pamoja na kosa la kula njama za kufanya kosa la ugaidi.
Kesi hiyo inayowakabili wanachama 17 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga imeahirishwa hadi Agosti 17, 2026 .
Uamuzi huo umetolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Glory Mwakihaba, ambapo washitakiwa walifikishwa mahakamani kwa mara ya pili tangu waliposomewa mashitaka kwa mara ya kwanza Julai 24, 2026.
Kwa mujibu wa mashitaka yanayowakabili, wanachama hao 17 wanadaiwa kuhusika na makosa yanayohusiana na ugaidi. Kati yao, Jackson Mnyawami ambaye ni Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Daniel Athuman na Jackson Kabyeseleza wanakabiliwa na shtaka la kupanga kufanya vitendo vya kigaidi, huku washitakiwa wengine 14 wakishtakiwa kwa kosa la kula njama za kufanya ugaidi.
Upande wa Jamhuri, unaowakilishwa na mawakili Joseph Mwakasege, Leonard Kiwango na Nyamnyaga Magoti, uliieleza mahakama kuwa uchunguzi wa shauri hilo bado haujakamilika, jambo lililopelekea mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 17, 2026 kwa hatua zaidi.
Washitakiwa wanatetewa na jopo la mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, wakishirikiana na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Wakili Gaston Kalubindi, pamoja , Wakili Alex Massaba na Gloria Ulomy.
Baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa John Heche amesema chama hicho kimepokea kwa masikitiko kukamatwa kwa wanachama wake, akiwemo Katibu wa Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, na kusisitiza matarajio yao kuwa mchakato wa kesi hiyo utaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya haki.

.jpeg)
