Mkuu wa Ubunifu wa Mikakati na Chapa wa Jambo Group ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Jambo Media, Nickson George akisaini mkataba wa kuidhamini Singida Black Stars.
Na Stella Herman, Shinyanga
Klabu ya soka ya Singida Black Stars imeingia makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja na kampuni ya Jambo Group kwa ajili ya msimu wa 2026/2027 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League) ambao tayari umeshaanza.
Mkataba huo umesainiwa leo Septemba 18, 2026, katika ofisi za Jambo Group zilizopo Shinyanga Mjini, ukiwa na lengo la kuisaidia klabu hiyo kujiimarisha na kufanya vizuri zaidi ikiwa ni mwendelezo wa kampuni hiyo kutoa udhamini kwa timu mbalimbali zinazoshiriki ligi kuu.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Ubunifu wa Mikakati na Chapa wa Jambo Group ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Jambo Media, Nickson George, amesema kampuni hiyo imeamua kuingia katika makubaliano hayo ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa uwekezaji wake katika soka la ndani.
"Katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, tumeamua kuongeza ushirika na timu ya Singida Black Stars kwa kuidhamini kwa msimu mzima wa 2026/2027, na udhamini huu utadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja," amesema George.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Singida Black Stars, Tabitha Kidawawa ameishukuru Jambo Group kwa kujiunga na familia ya klabu hiyo akisema udhamini huo utaongeza chachu na nguvu katika timu kuelekea msimu mpya.
Amesema wanafuraha kuanzisha ushirika huo na Jambo Group, huku akibainisha kuwa Singida Black Stars imekuwa na uhusiano wa karibu na Shinyanga hivyo ushirikiano huo ni hatua nyingine ya kuimarisha mahusiano hayo.
"Ni furaha kubwa kukutana na Jambo Group na kuanzisha ushirika huu Singida Black Stars imekuwa familia moja na Shinyanga, hivyo tunaamini ushirikiano huu utakuwa na manufaa kwa pande zote," amesema Kidawawa.
Mpaka sasa Kampuni ya Jambo Group imedhamini timu nne ambazo zinashiliki ligi kuu Tanzania bara ikiwemo Dodoma Jiji Fc,Pamba Jiji Fc,Geita Gold na Singida Black Stars