
Katika video yenye sauti kali aliyoiposti hivi karibuni, Niffer ameonekana kutofurahishwa na tabia ya baadhi ya watu wanaotumia jina lake kwa manufaa yao binafsi, huku wakiharibu taswira ya biashara zake ambazo amezitolea jasho.
"Mmetumwa na Nani?"
Niffer amewahoji wanaofanya vitendo hivyo kama kuna watu wanawalipa fedha ili kumharibia, akisisitiza kuwa hataki "shobo" na mtu yeyote na anataka aachiwe afanye biashara zake kwa amani.
"Unaposti page yangu wewe kama nani? Wewe ni nani kwangu? Kama unataka kunisapoti, nisapoti katika biashara kwa kuposti video yote, lakini siyo kuposti upotoshaji. Mmetumwa nini?" alihoji Niffer kwa ukali.
Akaunti Kufungwa: "Sikio la Kufa Halisikii Dawa"
Niffer amethibitisha kuwa tayari baadhi ya watu wameshapoteza akaunti zao baada ya kuripotiwa , na amewatahadharisha wengine kuwa zoezi hilo linaendelea kama hawataacha kutumia video zake vibaya.
"Jana niliposti nikasema; kama umechukua video yangu ukaenda kuposti kwenye udaku au kupotosha maana ya kile nilichoposti, mtapoteza hizo akaunti. Kuna mdada ana kisebengo na mkaka yuko huko... mjifunze kuheshimu majina ya watu. Mimi siyo mjinga."
Fundisho la "Ndani": Niffer Siyo Yule wa Zamani
Akikumbushia kipindi alichopata changamoto za kisheria na "kuingia ndani" (mahabusu), Niffer amesema alichojifunza huko kinatosha na kwamba hataachia mtu yeyote achezee jina lake kwa manufaa ya udaku.
"Nilichojifunza kule (ndani) ni kuwa nisitegemee mtu atumie jina langu kwa manufaa yake binafsi. Stress tulizopata mwanzo zimeshatutosha. Ukichukua video yangu ukaenda kuweka maana nyingine, tutafikishana pabaya."
Ujumbe kwa Wateja na Mashabiki
Niffer ameweka wazi kuwa ana wateja (customers) na watu wanaomtazama kama mfano (role models), hivyo hataki maudhui yanayokatisha watu tamaa ya kufanya kazi. Amesema wakati akiwa kwenye matatizo, wateja wake walimfariji, lakini "wambea" hawakuwepo.
"Niacheni na biashara zangu. Hii serikali isingekuwa inaniamini isingenifungulia nifanye biashara. Mnaumia nini mimi kuwepo uraiani? ... mchuma janga hula na wa kwao."
Habari hii imepokelewa kwa hisia mseto mitandaoni, huku wafanyabiashara wenzake wakimpongeza kwa kulinda "brand" yake, huku wapenda udaku wakionywa kukaa mbali na maudhui ya mwanadada huyo ambaye kwa sasa hana mzaha kwenye biashara.