

Na Stella Herman,Shinyanga
Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema
Serikali haitakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote anayekwamisha utekelezaji wa
miradi ya maendeleo kwa maslahi binafsi, jambo linalosababisha wananchi
kuchelewa kupata huduma ilhali fedha tayari zimetolewa.
Mhita ametoa kauli hiyo alipokuwa
akizungumza na madiwani pamoja na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kishapu, akisisitiza kuwa si jambo linalokubalika kwa wananchi kuendelea kukosa
huduma baada ya changamoto zao kuwasilishwa na viongozi wao na Serikali
kuchukua hatua ya kutoa fedha.
Amesema lengo kuu la Serikali ni
kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa haraka
ili kuwawezesha kuondokana na matatizo yao na kusonga mbele kimaendeleo, huku
akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano katika kuijenga Halmashauri ya
Kishapu.
“Nendeni mkasimamie miradi ya
maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu ili kuondoa changamoto
zinazowakabili wananchi ambao ndio waliowapa dhamana ya kuwaongoza. Pale
panapokuwa na changamoto, toeni taarifa kwa Mkurugenzi ili hatua zichukuliwe,”
amesema Mhita.



Pia amewataka viongozi hao kuendelea
kubuni na kusimamia vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza ukusanyaji wa mapato
ya ndani, jambo litakaloongeza mchango wa asilimia kumi unaotokana na mapato
hayo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Mhita amesisitiza umuhimu wa
kusimamia zao la pamba, ambalo ni tegemeo kubwa kwa wakulima na chanzo muhimu
cha uchumi wa Halmashauri ya Kishapu.
“Mna dhamana kubwa ya kusimamia zao
la pamba ili liendelee kuipa heshima Halmashauri yetu ya Kishapu. Hakuna sababu
ya sisi kutosonga mbele, maana hili ni zao letu kubwa la biashara,”
amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu, Josephat Limbe, amesema viongozi wa Halmashauri hiyo watatekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha watumishi wazembe wanaokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mamlaka husika, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.




















