UJENZI KITUO CHA AFYA MASAGALA WAPIGA HATUA, RC MHITA ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akikagua ujenzi wa Kituo cha afya Masagala Kata ya Maganzo Wilaya ya Kishapu

Na Johnson James, KISHAPU

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameonesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Masagala, kinachojengwa katika Kijiji cha Masagala, Kata ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu, kwa ufadhili wa Kampuni ya Mwadui kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) na nguvu za wananchi.

Akizungumza Januari 10, 2026, wakati wa ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa ujenzi huo, Mhe. Mhita alisema mradi huo ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na jamii katika kuimarisha huduma za afya na kupunguza adha kwa wananchi.

“Nimeridhishwa sana na kasi na ubora wa ujenzi wa kituo hiki. Hii ni jitihada kubwa na ya kuigwa, kwani wananchi walikuwa wanatembea hadi kilomita 20 kufuata huduma za afya,” alisema RC Mhita.

Awali, akitoa taarifa mwakilishi wa Mgodi wa WDL Sylivia  Mulogo amesema  jumla ya shilingi milioni 177 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa kituo hicho. Majengo yanayojengwa ni OPD, Maabara, RCH, kichomea taka, na vyoo vya matundu matano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Masagala, Bw. Juma Kapima, alisema kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wananchi waliokuwa wakifuata huduma Hospitali ya Kolandoto au Hospitali ya Mwadui.

Mkazi wa kijiji hicho, Bi. Doroth Balibusa, alisema wanawake wajawazito wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kujifungulia njiani, lakini sasa wana matumaini makubwa baada ya huduma kuletwa karibu nao.

Kituo cha Afya Masagala kinatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2026 na kuhudumia zaidi ya wananchi 22,000 kutoka vijiji vya jirani. 

 Mkuu wa Mkoa akiwa na viongozi wengine na baadhi ya wananchi mbele ya jengo la Kituo cha Afya Masagala


Post a Comment