Vitu vimetolewa nje baada ya nyumba kubomolewa
Na Stella Herman,ShinyangaMgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 18 katika Mtaa wa Ibinzamata, Manispaa ya Shinyanga, umefikia tamati baada ya mahakama kuamuru kuvunjwa kwa nyumba iliyokuwa imejengwa katika eneo linalodaiwa kuvamiwa, hatua iliyoambatana na kuondolewa kwa mali zilizokuwemo ndani.
Utekelezaji wa uamuzi huo umefanyika chini ya uangalizi wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akishirikiana na askari pamoja na viongozi wa serikali za Mtaa waliokuwa wakihakikisha taratibu zote zinafuatwa.
Chanzo cha mgogoro huo kilianzia mwaka 2007 baada ya Boaz Mwaipopo kudai umiliki wa eneo hilo na kujenga nyumba, madai ambayo yalipingwa na familia ya Kulinga, wakieleza kuwa ardhi hiyo ni mali ya Dotto Pamela Zakaria Kulinga tangu mwaka 1992.
Akizungumza baada ya utekelezaji huo, Baraka Chande Kulinga amesema licha ya kuwa na nyaraka halali za umiliki, walilazimika kupitia mchakato mrefu wa kisheria ili kuthibitisha haki yao, akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa wa sheria za ardhi.
Alibainisha kuwa mahakama ilitoa agizo Mei 16, 2025 likimtaka Mwaipopo kuondoka ndani ya siku 14, lakini alishindwa kutekeleza amri hiyo na kuendelea kuishi katika eneo hilo hadi ilipofikiwa hatua ya kuondolewa kwa nguvu kwa mujibu wa sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza eneo la tukio wakati wa kukabidhi eneo hilo kwa mmiliki halali.
Kwa upande wake, Mtatiro amesisitiza kuwa uvamizi wa ardhi ni kosa linalokiuka sheria na kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanaokiuka taratibu, akiongeza kuwa baadhi ya migogoro huchochewa na upungufu wa uadilifu kwa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibinzamata, Mohamed Mgendi, amesema juhudi zilifanyika kumtaka mhusika afike siku ya utekelezaji bila mafanikio, na baada ya operesheni hiyo kukamilika, eneo hilo lilikabidhiwa rasmi kwa familia ya mmiliki halali kupitia msimamizi wao Baraka Kulinga.
Baraka Kulinga msimamizi wa eneo la familia ambaye amekabidhiwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga baada ya kushinda kesi Mahakamani tangu Mei, 16 ,2025
Baraka Kulinga msimamizi wa eneo la familia 