
Safari ya abiria waliokuwa wakielekea mkoani Geita imekatishwa ghafla baada ya basi la kampuni ya OG Classic, lenye namba T985 DXL aina ya TATA, kupata ajali katika eneo la Wendele, Manispaa ya Kahama, na kusababisha vifo vya watu sita huku wengine watano wakijeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi,
Juni 20, 2026, majira ya saa 12:00 asubuhi, wakati basi hilo lilipokuwa
likisafiri kutoka Kahama kuelekea Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,
Janeth Magomi, amesema uchunguzi
wa awali unaonyesha kuwa dereva wa basi alifanya jaribio la kulipita lori
lililokuwa likielekea Masumbwe bila kuhakikisha mazingira yalikuwa salama.
Amefafanua kuwa baada ya kuanza
kulipita lori hilo, dereva alishindwa kulimudu basi kutokana na mwendo kasi,
likagonga ukingo wa barabara, kisha likarudi barabarani na kugonga tela la lori
kabla ya kupinduka.
"Taarifa za awali zinaonyesha
dereva alikuwa katika mwendokasi. Alipojaribu kulipita lori bila tahadhari,
aligonga ukingo wa barabara, akapoteza mwelekeo na hatimaye kugonga tela la
lori kabla ya basi kupinduka," amesema Kamanda Magomi.
Majeruhi wanaendelea kupatiwa
matibabu, huku miili ya waliofariki ikihifadhiwa kusubiri utambuzi wa ndugu na
taratibu za mazishi.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa
madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan kuepuka
mwendokasi na kufanya maamuzi ya tahadhari wanapolipita magari mengine, ili
kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya watu.