CHUO CHA SAYANSI ZA AFYA KOLANDOTO KUONGEZA WATAALAMU WA AFYA WENYE WELEDI ,KUPANDISHWA HADHI KUWA CHUO KIKUU

Baadhi ya wahitimu kutoka chuo cha sayansi za afya Kolandoto wakiwa kwenye mahafali ya 69 ya chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Dkt. Joseph Mayala
Na Stella Herman,Shinyanga

Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kimeendelea kupanua mchango wake katika sekta ya afya nchini, huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka kutoka 12 wakati chuo kinaanzishwa hadi kufikia 3,350 kwa sasa.

Kutokana na ongezeko hilo, Bodi ya Wadhamini ya chuo hicho imeitaka menejimenti kuharakisha mchakato wa kukipandisha hadhi kuwa chuo kikuu, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa udahili na kuzalisha wataalamu wengi zaidi wa afya kulingana na mahitaji ya soko la ajira nchini.

Akizungumza katika Mahafali ya 69 ya Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Dkt. Joseph Mayala, amesema kupandishwa hadhi kwa chuo hicho kutakiwezesha kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopokelewa na hivyo kuongeza mchango wake katika kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali za afya.

Dkt. Mayala amesema Serikali pia imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami inayounganisha barabara kuu na chuo hicho, pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi katika Kata ya Kolandoto, katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utarahisisha usafiri na upatikanaji wa huduma, hususan kwa wagonjwa wanaopelekwa katika Hospitali ya Kolandoto, huku kituo cha polisi kikitarajiwa kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Paschal Shiluka, amesema ongezeko la idadi ya wanafunzi ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uendeshaji wa chuo hicho na limekuwa mchango muhimu wa Kanisa la AICT katika kuzalisha wataalamu wa afya nchini.

Shiluka ameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo, akisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto za uhalifu ambazo zimekuwa zikikabili eneo hilo kwa muda mrefu.

Aidha, ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha hospitali na chuo hicho ili kurahisisha usafiri na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wanafunzi, wagonjwa na wananchi wanaofika katika eneo hilo.

Amesema Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kimeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya na elimu nchini, huku kikitoa mafunzo yanayolenga kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kuhudumia jamii.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 191 wametunukiwa vyeti katika ngazi za astashahada na shahada.

Wahitimu hao wamehimizwa kutumia elimu na ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii, kuzingatia maadili ya taaluma zao, kutii sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi, ambavyo vimeendelea kuwa miongoni mwa changamoto
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa AICT, Josephales Mtembe, amesema tangu kuanzishwa kwake, Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kimepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwemo kuongezeka kwa programu za masomo kutoka moja hadi saba.
Mtembe amesema Kanisa la AICT limeendelea kuchangia maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya na maendeleo ya jamii, kwa kuanzisha na kusimamia miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Katibu Mkuu wa AICT, Josephales Mtembe


Post a Comment