YOUNG WOMEN LEADERSHIP YATAMBULISHA MRADI WA KUWAJENGEA UWEZO WANAWAKE VIJANA

 

     Meneja miradi kutoka Shirika la Young Women Leadership Veronica Masawe akizungumza na viongozi wa Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga wakati wa kutambulisha mradi wa Mwanamke ni sehemu ya maamuzi shiriki naye utakaotekelezwa Kata ya Kizumbi na Mwawaza

Na Stella Herman,Shinyanga

Shirika la Young Women Leadership limetambulisha rasmi mradi wake wa “Mwanamke ni sehemu ya maamuzi shiriki naye” utakao tekelezwa katika Kata ya Kizumbi na Mwawaza Manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana wanawake kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35.

Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi huo leo Septemba 9,2026 kwa viongozi wa Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga,Meneja miradi kutoka Shirika la Young Women Leadership Veronica Masawe,amesema mradi huo utasaidia kuwawezesha wanawake vijana kutumia fursa za maamuzi zilizopo katika maeneo yao na kushiriki fursa za kiuchumi.

Amesema kupitia mradi huo utawajengea uwezo kupinga vitendo vya rushwa ya ngono,kushirika fursa za kijamii na vyombo mbalimbali vya maamuzi kuanzia ngazi ya familia,ambapo katika kata zote mradi utafika kwenye vijiji vitatu kila Kata ambapo pia utahusisha makundi mbalimbali kulingana na shuhuli itakayotekelezwa.

“Kundi hili la wanawake vijana ndilo ambalo linakumbana na changamoto nyingi katika Jamii na ndiyo maana tumeleta mradi huu ili kuwawezesha wanawake vijana kupatiwa elimu ya masuala mbalimbali ili kuwajenga na kuwawezesha kuwania nafasi mbalimbali zinazotokea katika Jamii”amesema Masawe

“Mradi huu umelenga kuwafikia zaidi ya wanawake vijana 180 katika Kata zote mbili katika vijiji sita na idadi itaongezeka kadri mradi unavyoendelea kutekelezwa ,hatua hii itawawezesha kuwawezesha kujiamini,kujitegemea na kuwa na maamuzi”amesema Masawe

Mradi huu umefadhiliwa na mfadhili Global Affairs Canada(GAC),mshirika mkuu anayesimamia utekelezaji Cuso International na Washirika wa kimkakati katika utekelezaji wa mradi ambao ni Msichana Initiatives,Women Fund Tanzania Trust na Tanzania Health Forum Initiative.
Mwakilishi wa kundi la wanawake vijana Scholastika Maganga amelishukuru shirika la Young Women Leadership kwa kulikumbuka kundi hilo ambalo limekuwa likipitia mambo mengi,ambapo elimu watakayoipata itawajenga kuwa na ujasiri na kujiamini.

Kwa upande wake Mtemi Kidola wa pili Charles Njange amesema mradi huo umefika muda muafaka ambao utawajenga kuwa na ujasiri,kujiamini na kujithamini pia kuwa na uthubutu wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zinapotokea pia kupata mbinu za kujiepusha na vishawishi wanavyokumbana navyo.

Diwani wa Kata ya Kizumbi Reuben Kitinya akichangia mada wakati wa kutambulisha mradi wa “Mwanamke ni sehemu ya maamuzi shiriki naye” 






Post a Comment