
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutoa elimu kwa walipakodi kuhusu sheria mpya inayohusu msamaha wa miezi 12, huku ikiwahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kodi.
Elimu hiyo inatolewa kupitia ushiriki wa TRA katika maonyesho, ambapo wananchi wanapata fursa ya kukutana moja kwa moja na maafisa wa mamlaka hiyo na kupata majibu ya maswali yao kuhusu kodi.
Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Justine Katiti, amesema ushiriki wao katika maonyesho hayo unalenga kuwafikia wananchi kwa urahisi na kuwapatia elimu sahihi kuhusu wajibu wao kama walipakodi.
“Tunashiriki katika maonyesho haya kwa lengo la kutoa elimu kuhusu sheria mbalimbali za kodi, ikiwemo sheria mpya inayohusu msamaha wa miezi 12. Wananchi wanapata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wetu,” amesema Katiti.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la TRA wamepongeza hatua hiyo, wakisema elimu inayotolewa imewasaidia kuondoa hofu na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kodi, huku uwepo wa maafisa hao katika maonyesho ukiwawezesha kupata huduma na ufafanuzi kwa urahisi.


