BALINA YANG'ARA MATOKEO DARASA LA SABA WANAFUNZI WOTE 48 WAPATA UFAULU WA ASILIMIA 100

Na Stella Herman, Shinyanga

SHULE ya Msingi Balina imeendelea kuonesha kiwango kizuri cha ufaulu katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026, baada ya wanafunzi wote 48 waliofanya mtihani huo kufaulu na kuipa shule wastani wa alama 248.3125, ulioweka shule hiyo katika daraja A (Bora).
Matokeo hayo yanaonesha kuwa kati ya wanafunzi hao, 34 wamepata daraja A, huku wanafunzi 14 wakipata daraja B, bila kuwapo mwanafunzi aliyepata daraja C, D au E.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), ufaulu huo umejumuisha wavulana 24 na wasichana 24, ambapo wasichana 12 wamepata daraja A na 12 daraja B, huku wavulana 22 wakipata daraja A na wawili daraja B.

Uchambuzi wa matokeo katika masomo sita yaliyofanyiwa tathmini unaonesha kuwa shule hiyo imefanya vizuri zaidi katika somo la Kiingereza, lililopata wastani wa alama 45.6458 na daraja A.

Somo la Kiswahili limefuatia kwa wastani wa alama 44, likipata daraja A, huku Hisabati likipata wastani wa alama 42.3750 na daraja A.
Katika masomo mengine, Uraia na Maadili limepata wastani wa alama 40.3333, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi likipata alama 39.0417 na Sayansi na Teknolojia likipata wastani wa alama 36.9187, yote yakiwa katika daraja B.

Matokeo hayo yanaifanya Shule ya Msingi Balina kuwa miongoni mwa shule zilizoweka alama nzuri katika mtihani huo, huku ufaulu wa asilimia 100 ukiwa ni kielelezo cha matokeo yaliyopatikana kwa wanafunzi wote waliofanya mtihani.

Mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuweka mikakati ya kuinua ufaulu katika masomo yote ili wanafunzi wengi zaidi waweze kufikia kiwango cha juu cha ufaulu.

Post a Comment