RUJAT YAINGIA KIDIJITALI, YAZINDUA TOVUTI RASMI KWA HABARI ZA VIJIJINI

Na Stella Herman, Dodoma

Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT) kimezindua rasmi tovuti yake ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi na kuchangia katika kuharakisha maendeleo ya jamii.

Akizindua tovuti ya (RUJAT) yenye anuani ya www.rujat.or.tz Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati wa Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho amewataka waandishi wa habari kulifikia kundi kubwa lililopo vijijini.

Msigwa amewataka waandishi wa habari kupaza sauti za wananchi wanaoishi vijijini na kuwasaidia kupata taarifa sahihi pamoja na kuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili katika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi na mamlaka husika.

Msigwa ameipongeza RUJAT kwa hatua hiyo, akieleza kuwa tovuti hiyo itarahisisha upatikanaji wa habari, taarifa mbalimbali na kuchangia katika kuharakisha maendeleo ya jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Akizungumza kwenye kongamano hilo Mbunge wa Bunda Mjini na mwanahabari mwandamizi Ester Bulaya, amewataka waandishi kurejea misingi ya uandishi wa habari iliyokuwa ikitumika miaka ya nyuma, ikiwemo kufanya utafiti, kuchunguza taarifa kabla ya kuzichapisha na kuongeza ubunifu.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya RUJAT kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, Katibu wa Chama hicho Prosper Kwigize, amesema kuanzishwa kwa tovuti hiyo ni miongoni mwa mafanikio muhimu yaliyopatikana katika kipindi hicho.
“ Katika safari ya kukua na kuimarika kwa Chama hatua kubwa ya mafanikio ni kufungua tovuti yetu ukizingatia katika zama ambazo teknolojia ya habari na mawasiliano ina nafasi kubwa ya kujenga taasisi imara na kuunganisha wadau” amesema Kwigize

Amesema tovuti hiyo inalenga kuimarisha utambulisho wa RUJAT katika majukwaa ya kidijitali, kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu Chama na shughuli zake, pamoja na kuongeza mwonekano wake kwa wanachama, taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, washirika wa kimataifa na umma kwa ujumla.




Post a Comment