
Wananchi wa Kijiji cha Nyambula Kata ya Ngogwa Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wameungana pamoja kuchangia fedha, vifaa vya ujenzi na nguvu kazi kwa ajili ya kujenga shule ya sekondari nyambula huku wakiiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuwaunga mkono ili kukamilisha mradi huo.
Hatua hiyo ya wananchi inalenga kuondoa adha wanayoipata watoto wao kutembea umbali wa kilomita 24 kwenda na kurudi shuleni kutoka Kijijini cha Nyambula hadi Shule ya Sekondari Ngogwa umekuwa kikwazo kwa baadhi ya wanafunzi kuendelea na masomo kutokana na kutembea umbali mrefu huku wanafunzi wa kike wakikabiliwa na vishawishi na changamoto mbalimbali njiani hali inayohatarisha mstakabali wao wa elimu.
Wamesema hali hiyo pia imekuwa chanzo cha wasiwasi kwa wazaz, kuhusu usalama wa watoto wao wa kike ambao hukumbana na changamoto mbalimbali wanapotembea umbali mrefu kuelekea shuleni.
Wamesema uamuzi wa kuanzisha ujenzi wa shule hiyo umetokana na kuona umuhimu wa kusogeza huduma za elimu karibu na makazi yao ili kuwapa watoto nafasi nzuri ya kutimiza ndoto zao.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi wengine mkazi wa kijiji cha Nyambula wakati wa kazi ya ujenzi wa msingi wa nyumba vya madarasa ikiendelea ,Kasimu Mabuga amesema wameamua kuungana na viongozi wa kijiji pamoja na diwani kuanzisha mradi huo baada ya kubaini kuwa umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni umekuwa tatizo kubwa kwa watoto wao.
Amesema baadhi ya wanafunzi hulazimika kupita katika maeneo yenye mazingira magumu ambapo kutokana na changamoto hiyo na kuona umuhimu wa elimu ,yeye binafsi Mabuga amechangia Sh 100,000 na kuwataka wananchi wengine pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia ili ujenzi huo ukamilike.
Kwa upande wake Arnold Jovin amesema wanafunzi wengine wamekuwa wakiishia njiani na wakati mwingine kushindwa kufika shuleni kutokana na umbali mrefu wanaotembea, hali inayozidi kuwa ngumu na kushindwa kufikia ndoto zao.


Amesema wananchi wameupokea kwa furaha mradi huo na kuiomba Serikali kusaidia kukamilisha miundombinu inayohitajika ili watoto wapate elimu katika mazingira yaliyo salama na rafiki.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Njiapanda Shija Mhoja Manyanda, amesema wananchi na viongozi walikaa pamoja na kujadili changamoto hiyo kabla ya kufikia uamuzi wa kuanzisha ujenzi wa shule kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Amesema wameanza kujichangisha kwa nguvu zao wenyewe, lakini bado wanahitaji msaada wa Serikali ili kukamilisha ujenzi na kuiwezesha shule hiyo kuanza kutoa huduma.
Akifafanua kuhusu kuanzishwa kwa mradi huo Diwani wa Kata ya Ngogwa, Abel Mabao amesema wazo la kujenga shule hiyo lilitokana na kubaini kuwa wanafunzi wa Nyambula wanalazimika kutembea kilomita 12 kwenda na kilomita 12 kurudi katika Shule ya Sekondari Ngogwa.
Amesema hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo, huku watoto wa kike wakikabiliwa na changamoto za usalama na vishawishi vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wao wa elimu.
Mabao amesema hadi sasa wananchi wamefanikiwa kujenga msingi wa madarasa manne na ofisi moja, hatua iliyofikiwa kupitia michango ya fedha, vifaa vya ujenzi na nguvu kazi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.



Ameeleza kuwa wananchi wamechangia takribani Shilingi milioni 1.2, huku yeye binafsi akichangia Shilingi milioni tano kuunga mkono juhudi hizo.
Aidha, amesema mradi huo umepokea michango ya vifaa vya ujenzi, ikiwemo mifuko ya saruji pamoja na matofali 1,100 ambayo tayari yamepatikana kwa ajili ya kuendeleza ujenzi.
Diwani huyo amesema mafundi wanaoshiriki katika ujenzi huo wanatoka ndani ya kijiji, akieleza kuwa ana mpango wa kuwaunganisha katika kikundi kitakachowawezesha kusajiliwa kwenye mfumo wa NEST ili wapate fursa za kushiriki katika kazi mbalimbali za ujenzi ndani ya Manispaa ya Kahama.
Pamoja na hatua iliyofikiwa, Mabao ameiomba Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia kukamilisha mradi huo, akieleza kuwa ushirikiano wao utakuwa muhimu katika kuhakikisha shule hiyo inaanza kutoa huduma kwa watoto wa Nyambula na vijiji jirani .
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)