Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa wito kwa wananchi kusherehekea sikukuu ya mwisho wa mwaka na kuukaribisha mwaka mpya kwa kuzingatia sheria na kuzingatia kanuni za kiusalama, likisisitiza kuwa imara katika kuimarisha usalama kwa misingi ya sheria.
Aidha Polisi imetoa rai kwa kila mzazi kuzingatia ulinzi kwa watoto kama sheria, kanuni na taratibu zinavyoelekeza ili kuwaepusha na madhara mbalimbali ikiwemo kupotea kama ilivyoshuhudiwa katika sikukuu nyingine zilizopita.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania David Misime kwa Vyombo vya habari imesisitiza pia kwa watumiaji wa Vyombo vya moto na watumiaji wa barabara kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani na kuongozwa na kaulimbiu ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani isemayo "Familia yako inakusubiri zingatia usalama."
"Kulingana na desturi zetu kama Watanzania huwa tunakuwa na shughuli mbalimbali katika kuhitimisha mwaka na kuukaribisha mwaka mpya ikiwemo kushiriki kwenye mikusanyiko ya kumwomba na kumshukuru Mungu kwenye nyumba za ibada na wengi huka na familia, ndugu, na marafiki na kusherehekea aidha majumbani au sehemu wanazoona zinafaa kufanya hivyo."
Ili hayo matumainu ya kila mmoja wetu na shughuli hizo ziweze kufanyika bila hofu, au wasiwasi, amani, utulivu na uaalama lazima uwepo. Kwa mantiki hiyo Jeshi la Polisi linatoa wito ili kila mmoja aweze kusherehekea sikukuu hizi kwa namna anavyoona inafaa ili mradi havunji sheria ni wajibu wa kila mmoja kuzingatia kanuni za kiusalama kwani usalama huanza na wewe kwanza." Amesema David Misime.
Polisi pia kupitia kwa Msemaji wake David Misime imebainisha kuwa kwa wale waliomba vibali vya kupiga fataki na wakaruhusiwa, wametakiwa kuzingatia maelekezo na muda waliopewa ili kuepuka usumbufu kwao na kwa wengine hasa wagonjwa,Polisi pia ikipiga marufuku uchomaji wa matairi.
