
Tanzania inashuhudia mapinduzi makubwa ya kiuchumi ambayo hayajawahi kutokea. Takwimu za Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA ) zilizowasilishwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, zinaonyesha kuwa nchi yetu imevunja rekodi kwa kusajili miradi 915 yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 10.9.
Huu ni ushindi kwa kila Mtanzania kwani miradi hii inakwenda kuzalisha ajira zaidi ya 161,000.
Lakini, katikati ya neema hii, kuna kundi la watu wachache, wakiongozwa na akina Maria Sarungi na wenzake, wanaonekana kukerwa na utulivu huu na sasa wanapika njama za kuleta vurugu ifikapo Januari Mosi.
Inasikitisha kuona kuwa wakati serikali na wawekezaji wanapambana kufungua viwanda kama MCGA Auto na Canal Industries ili vijana wapate kazi, kuna watu wako bize kwenye mitandao na vyumba vya siri wakipanga namna ya kubomoa amani ya Tanzania.
Hawa ni watu waliojawa na maslahi binafsi ambao hawaoni fahari kuona mabilioni ya fedha yakimiminika nchini, bali wanatamani kuona taharuki na damu zikimwagika mtaani. Wanachochea hasira kwa vijana ili kufuata mikumbo, huku wao na familia zao wakiwa wamejificha kwenye usalama wa kuta zao, wakisubiri kutumia ghasia hizo kama mtaji wa kiuchumi na wengine kisiasa.
Tunapaswa kujiuliza: Ni nani anafaidika amani ikitoweka? Jibu ni rahisi—ni wale wote wasioitakia mema Tanzania. Mwekezaji hawezi kuleta dola milioni 50 kwenye nchi yenye vurugu. Ukivuruga amani Januari Mosi, unakuwa umefuta ajira za wale vijana 161,000 waliokuwa na matumaini ya kuanza mwaka mpya kwa neema.
Huu ni usaliti wa hali ya juu kwa taifa. Akina Maria Sarungi na wenzake lazima waelewe kuwa Tanzania ni kubwa kuliko ajenda zao za chuki, na Watanzania wa leo si wa kudanganywa na kufuata mkumbo wa vurugu unaolenga kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo.
Sauti za busara kutoka kwa viongozi wa mitaa na mafundi mbalimbali huko Kibaha zinatukumbusha kuwa amani ni tunu kutoka kwa Mungu na ndiyo ngao yetu kuu. Wazazi wanapaswa kuwaonya watoto wao dhidi ya kutumiwa na watu hawa ambao wameshindwa hoja na sasa wanatafuta kufanya fujo.
Tunapaswa kuchagua busara na mazungumzo badala ya kufuata maelekezo ya watu wanaotaka kututia doa kitaifa na kimataifa. Tanzania ina amani, na ndiyo maana hata mastaa wakubwa kama Kanye West wanatamani kuja kupanda Kilimanjaro; tusiwaruhusu wachache wenye njaa ya madaraka waharibu taswira hii nzuri.
Tunawaomba viongozi wa dini na taasisi zote za kijamii kukemea vikali njama hizi za Januari Mosi. Nguvu ya vijana itumike kujenga viwanda na kukuza teknolojia, si kubomoa kile tulichokijenga kwa miongo mingi.
Sisi tunaopenda amani ni wengi, na sauti yetu ya mshikamano ni kubwa kuliko kelele za wachochezi. Tuchague kulinda urithi wetu, tuchague kulinda ajira zetu, na tuchague kuivusha Tanzania salama kuelekea mwaka 2026 tukiwa wamoja na imara.