ZAIDI YA VIJANA 600 WATEMBEA KWA AMANI KUONESHA FAHARI YA KISAFWA

 

Taswira ya amani na utulivu imetawala katika mji wa mpakani wa Tunduma, mkoani Songwe, baada ya zaidi ya vijana 600 wa kabila la Wasafwa kufanya matembezi makubwa ya kitamaduni yaliyopambwa na nyimbo, ngoma, na shamrashamra za kipekee.

Tukio hilo lililofanyika Desemba 2025, limekuwa kielelezo tosha kuwa amani ndiyo msingi wa furaha. Bila utulivu uliopo nchini, isingewezekana kwa kundi kubwa la vijana kukusanyika, kufunga barabara kwa muda kwa amani, na kuonesha utajiri wa asili yao bila hofu yoyote.

Baraka  Thomson Mwashobezya, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kisafwa Tunduma amesema maandamano yao ya amani ya kuenzi utamaduni na ushirikiano yamewezekana kutokana na amani iliyopo na kusihi vijana wenzake kutambua umuhimu wa amani katika maisha na katika shughuki zao za kujiletea maendeleo.

Alisema umoja huo wenye wanachama zaidi ya 600 umeundwa kuhamasisha kujitambua na kushikamana, kukosoana na kusaidiana ili vijana wasonge mbele kimaendelkeo na kijamiii.

Ujumbe wa Amani na Kazi

Maadhimisho hayo ya kutimiza mwaka mmoja wa umoja wa vijana hao yamebeba jumbe nzito zenye mwelekeo wa kijamii na kiuchumi:

Dawa ya Umasikini ni Kazi 

Moja ya kauli mbiu zilizovuma katika tukio hilo ni "Idawa yi yipina wawombe mbombo", ikiwa na maana ya kuhimiza vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi, jambo ambalo linawezekana tu palipo na utulivu.

Kuenzi Utamaduni

Vijana hao wameonesha kuwa amani inatoa fursa kwa vizazi vipya kujivunia lugha na asili yao. Hii inajenga utambulisho wa Taifa na kuzuia mmomonyoko wa maadili.

Mshikamano wa Makabila 

Licha ya kuwa ni sherehe ya Wasafwa, wadau kutoka makabila mengine kama Wanyakyusa wameonekana kuunga mkono na kufurahia ngoma hizo, jambo linalothibitisha kuwa Tanzania ni nchi ya umoja na mapatano.

Tusiharibu Amani Yetu

Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanabainisha kuwa matukio kama haya ya Tunduma ni ukumbusho kwa kila Mtanzania kuwa amani ni tunu isiyopaswa kuchezewa.

"Tunapata fursa ya kucheza, kuimba, na kusherehekea umoja wetu kwa sababu nchi iko salama. Tukiharibu amani, hata hizi ngoma za asili na furaha tuliyonayo leo vitatoweka," alisema mmoja wa waandaaji wa matembezi hayo.

Maoni ya Wananchi

Mitandao ya kijamii imelipuka kwa furaha huku watu wengi wakipongeza hatua hiyo ya vijana wa Kisafwa. Wengi wamesisitiza kuwa kuona vijana wanajivunia asili yao (Wasafwa Hoyeee!) ni ishara ya taifa linalojitambua na linaloishi kwa upendo.

Tukio la Tunduma ni somo kuwa amani si neno tu, bali ni mazingira yanayoruhusu utamaduni kunawiri, vijana kufanya kazi, na jamii kuwa na furaha. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa chokochoko za aina yoyote hazivurugi uzuri huu wa Kitanzania. 

Post a Comment