
NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA
PROPHET Nicolaus Suguye ameahidi kutoa matofali elfu tatu pamoja na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Kituo cha Kahama Peace Orphanage Center, kilichopo Mtaa wa Dodoma Viwandani, Kata ya Zongomela, Manispaa ya Kahama.
Ahadi hiyo ameitoa leo Septemba 8, 2026, baada ya uongozi wa kituo hicho kueleza changamoto ya ukosefu wa uzio, ambao umekuwa ukihatarisha usalama wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi wa Kahama Peace Orphanage Center, Abubakari Issa, amesema ukosefu wa uzio ni changamoto kubwa kwa kituo hicho, kutokana na baadhi ya watoto kutoka nje na kukutana na mazingira ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
Issa amesema kituo hicho tayari kimeanza kuweka msingi wa ujenzi wa uzio, lakini kimekuwa kikihitaji msaada wa vifaa ili kukamilisha kazi hiyo.
“Watoto wetu amekuwa wanapotea, watoto wetu walikuwa wanakutana na mambo yabkuhatarisha usalama wao kama kung'atwa na mbwa kutokana na ukosefu wa uzio, lakini kwa sababu Prophet Suguye amekuja na ameelewa changamoto yetu, sina shaka kwamba watatusaidia,” amesema Issa.
Amesema ujenzi wa uzio utasaidia kuboresha usalama wa watoto na kuwezesha kituo kuendelea kutoa malezi katika mazingira salama kwanibwanapokea watoto wadogo mpaka chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake, Prophet Suguye amesema jamii ina wajibu wa kushirikiana katika kuwasaidia watoto wenye uhitaji, akisisitiza kuwa msaada haupaswi kuishia kwenye chakula pekee, bali pia kuangalia mahitaji mengine muhimu yanayoweza kuboresha maisha na mustakabali wa watoto hao.
Mbali na Kahama Peace Orphanage Center, Suguye ametembelea pia New Hope Orphanage Center, kilichopo Mtaa wa Mwime, Kata ya Zongomela, ambapo ametoa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Miongoni mwa mahitaji hayo ni sukari, maharage, sabuni, mafuta ya kupikia, unga wa sembe pamoja na mahitaji mengine ya matumizi ya kila siku.
Msimamizi wa New Hope Orphanage Center, Scolastika Fred, amesema kituo hicho kinatoa malezi pamoja na elimu kwa watoto wenye uhitaji, kuanzia shule ya msingi hadi ngazi ya chuo kikuu.
“Tuna kituo kinachotoa malezi pamoja na elimu kwa watoto wenye uhitaji kusoma, kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu. Tunashukuru sana kwa ujio wenu, tunaomba Mungu awabariki na awaongezee kila siku,” amesema Scolastika.
Mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho Judith Suleman amemshukuru Suguye kwa msaada huo, akisema jamii ina nafasi kubwa katika kuwasaidia watoto wenye uhitaji.
Amesema licha ya changamoto wanazokutana nazo, baadhi ya watu wamekuwa wakijitolea kuwasaidia, jambo analoliona kuwa ni sehemu ya mshikamano wa jamii.
“Tunawashukuru sana hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuwaambia tunawashukuru, Mungu ambariki kila anayejitolea kutusaidia,” amesema mtoto huyo.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya shughuli za Suguye katika Manispaa ya Kahama kabla ya kuanza kwa mkutano wa injili unaotarajiwa kuanza kesho Septemba 9, 2026.















