AMANI KWANZA: SAUTI ZA WANANCHI DHIDI YA MIHEMKO YA KISIASA

Watanzania wamehimizwa kulinda amani, umoja, na mshikamano wa taifa kwa wivu mkubwa kama msingi pekee wa kujiletea maendeleo ya kweli, huku wakionywa kuwa pasipo utulivu hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana. 

Kauli hizi zimetolewa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, akiwemo Athumani Mkongota, mkazi wa Kibaha Mjini, ambaye amesisitiza kuwa mshikamano ndio nguzo inayolishikilia taifa. 

Mwelekeo huu wa kizalendo unakuja wakati ambapo mijadala ya kijamii imeongezeka kuhusu namna ya kudai haki bila kuhatarisha usalama, huku wananchi wakitakiwa kurudi katika kujitafakari na kuona ni kwa kiasi gani maisha yanaweza kubadilika na kuwa katika taharuki kubwa pindi amani inapotoweka.

Katika kile kinachoonekana kama funzo kutokana na matukio ya hivi karibuni, Daudi Inuka, mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, ametoa mwito wa kutafuta njia mbadala na bora za kudai haki badala ya kukimbilia vurugu ambazo mara nyingi huacha majeraha kwa jamii.

Maoni haya yanaungwa mkono na Musa Mseti ambaye amebainisha kuwa amani ndiyo kila kitu kwa sababu shughuli zote za kiuchumi na kijamii zinafanyika kwa ufanisi pale tu ambapo utulivu umetawala.

 Wananchi hao wamebainisha kuwa kushuhudia taharuki inayoweza kutokea kupitia vurugu kumejenga ufahamu mpya kuwa amani si jambo la kuchukulia mzaha, bali ni fursa muhimu inayopaswa kulindwa dhidi ya yeyote anayejaribu kuivuruga.

Mjadala huu umepata mwangwi mpana pia katika mitandao ya kijamii ambapo Watanzania wengi wameanza kuhoji nia ya mataifa ya nje, kama Marekani, wakiamini kuwa mataifa hayo mara nyingi huchochea vurugu nje ya ardhi yao huku yakilinda usalama wa ndani. 

Baadhi ya wachangiaji wamebainisha kuwa Tanzania ina akili nyingi na busara kuliko mataifa mengine mengi ya Afrika, na kwamba mabadiliko ya kweli yanapatikana kupitia maridhiano na njia za amani badala ya kufuata mikumbo ya vurugu. 

Hoja imekuwa ni kwamba, ingawa kuna madai ya haki au changamoto za kimaisha , njia ya kuivuruga nchi haijawahi kuwa suluhu ya kudumu, bali ni mtego unaoweza kumrudisha mwananchi nyuma kimaendeleo.

Hisia za wananchi zimejikita katika ukweli kuwa kufuata mikumbo ya kisiasa bila kutafakari kunaweza kuleta madhara makubwa kwa mtu mmoja mmoja. Watu wengi sasa wamechagua amani kama njia sahihi, wakiamini kuwa haki inaweza kupatikana bila kumwaga damu au kuharibu mali. 

Mwito uliotolewa kwa Watanzania wote ni kuendelea kuwa na uelewa mpana wa kijiopolitiki na kutambua kuwa kazi na utu ndizo silaha za kusonga mbele. Katika kipindi hiki cha mabadiliko, busara imeshinda mihemko, huku wananchi wakiazimia kusimama kidete kukataa ajenda zozote zinazolenga kuingiza taifa kwenye machafuko, wakitambua kuwa ukombozi wa kweli unajengwa juu ya misingi ya utulivu na siyo mabaki ya nchi iliyovurugika.

 

Post a Comment