TUME YA UCHUNGUZI MATUKIO YA UCHAGUZI YAZIDI KUPATA BARAKA ZA WAZEE, WASOMI NA WANASIASA

TUME ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Januari 14, 2026, imefanya mfululizo wa vikao vizito na viongozi waandamizi wastaafu, wanasiasa na wataalamu wa uchumi, ikiwa ni sehemu ya kutafuta tiba ya kudumu ya amani nchini.

Katika mfululizo wa mikutano hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ndani ya Ukumbi wa Tanganyika katika Jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume imekutana na kufanya majadiliano ya kina na Jaji Mstaafu Joseph Warioba, Mzee Joseph Butiku, pamoja na mwanasiasa January Makamba.

Mikutano hiyo imelenga kupata uzoefu wa viongozi hao katika masuala ya utulivu wa nchi, kuelewa namna vurugu hizo zilivyoanza, athari zilizojitokeza kwa watu na miundombinu, pamoja na kupokea ushauri wa kitaalamu wa namna ya kuzuia matukio hayo yasijirudie katika chaguzi zijazo.

Aidha, Tume hiyo pia imekutana na wataalamu wa uchumi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi. Ingawa haikutolewa taarifa rasmi,kwa asilin ya watu wa kariba waliyoitwa wanatarajiwa kueleza kwa kina namna uvunjifu wa amani ulivyotingisha misingi ya uchumi wa nchi, ikiwemo kudorora kwa shughuli za kibiashara na uharibifu wa mali za wananchi na umma wakati wa kipindi hicho cha uchaguzi na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa siasa za nchi haziwi kikwazo kwa ukuaji wa uchumi, bali ziwe kichocheo cha utulivu unaovutia uwekezaji.

Tume hii iliundwa kufuatia maelekezo ya Rais baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Uchaguzi huo, ingawa ulihitimishwa, uligubikwa na matukio ya hapa na pale ya uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo nchini, jambo ambalo liliibua hofu na kusababisha uharibifu wa mali na majeruhi kwa baadhi ya wananchi.

Lengo kuu la Serikali kuunda Tume hii ni kufanya uchunguzi wa kina na wa haki ili kupata 'kiini' cha machafuko hayo. Badala ya kulaumu, Tume imejikita katika kukusanya ushahidi, kusikiliza maoni ya wadau wote, na kutengeneza ripoti itakayotoa dira mpya ya kitaifa kuhusu namna ya kuendesha michakato ya kidemokrasia bila kuathiri umoja wa nchi.

Wito kwa Wananchi: Jitokezeni Kutoa Maoni

Kazi ya Tume hii haina tija kama wananchi, ambao ndio waathirika wakuu na mashuhuda wa matukio hayo, hawatashiriki. Tume inatoa wito kwa Watanzania kutoka makundi yote kuendelea kujitokeza kutoa ushuhuda na maoni yao.

Umuhimu wa wananchi kujitokeza unatokana na sababu zifuatazo:

Kutibiwa kwa Vidonda: Kutoa maoni ni sehemu ya mchakato wa maridhiano na kuponya mioyo ya walioumia.

Kusema Ukweli: Ili Tume ipate picha halisi ya nini kilitokea mitaani, inahitaji sauti ya mwananchi wa kawaida, si viongozi pekee.

Kulinda Baadaye: Maoni ya mwananchi wa leo ndiyo yatatengeneza sheria na taratibu zitakazomlinda mtoto wa Kitanzania katika uchaguzi wa mwaka 2030 na kuendelea.

Tume imesisitiza kuwa itaendelea kukutana na watu wa kada mbalimbali, wakiwemo waathirika wa moja kwa moja, ili kuhakikisha kuwa ripoti itakayowasilishwa inabeba hisia, ukweli, na matamanio ya Watanzania wote katika kudumisha amani iliyoachwa na waasisi wa taifa hili.

Post a Comment