
Matibabu ya kibingwa ya pua,koo na masikio yanatarajia kuwafikia zaidi ya wakazi elfu mbili kutoka Mkoa wa
Shinyanga na maeneo ya jirani ambao watanufaika na huduma hizo zilizoanza kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.Kuanza kwa huduma hiyo leo Januari
5,2026 ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na
wananchi ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Mikoa mingine na kuongeza
upatikanaji wa matibabu ya kitaalamu ndani ya Mkoa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
huduma hizo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nelson Mgaya, amesema kumekuwepo
na ongezeko la magonjwa ya koo kwa watoto wadogo pamoja na changamoto ya usikivu
hafifu kwa watu wazima, hatua ambayo inaashiria kuwepo kwa tatizo kubwa la
kiafya katika jamii.
Dkt. Mgaya amesema kuanza kwa
kliniki hiyo kutawawezesha wananchi kupata uchunguzi wa mapema, matibabu sahihi
pamoja na ushauri wa kitaalamu, huku akiwataka wakazi wa Shinyanga na mikoa ya
jirani kujitokeza kwa wingi kutumia huduma hizo.

Naye Mkuu wa Idara ya Upasuaji
katika hospitali hiyo, Dkt. Geofrey
Mboye, amesema hospitali imejipanga kikamilifu kwa kuwa na wataalamu wa
kutosha pamoja na vifaa tiba muhimu ili kuhakikisha huduma za pua, koo na
masikio zinatolewa kwa ufanisi na kwa usalama.
Baadhi ya wananchi walioanza
kunufaika na huduma hizo, akiwemo Magreth
Nyange, wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma za kibingwa karibu na
wananchi, ambapo wameeleza hatua hiyo itapunguza gharama na usumbufu wa
kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu katika mikoa mingine.