TANZANIA imeendelea kung’ara katika medani za kimataifa baada ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) mwaka 2026, hatua inayotajwa kuwa ni pigo kwa wanaharakati na mataifa majirani wasioitakia mema nchi, waliojaribu kupaka matope tasnia ya utalii nchini.
Hatua hiyo inakuja wakati taifa likishuhudia ongezeko kubwa la watalii na kuimarika kwa imani ya jumuiya ya kimataifa kwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Takwimu Zanyamazisha Wapinzani
Akizungumza Januari 17, 2026, jijini Dodoma katika kikao cha wadau wa sekta ya utalii na wanyamapori, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema uteuzi huo umetokana na rekodi za kutisha za mafanikio ambazo Tanzania imezipata kwa kipindi kifupi.
Dkt. Kijaji amebainisha kuwa kati ya Januari na Novemba 2025, idadi ya watalii iliongezeka kwa asilimia tisa, ambapo watalii 2,097,823 waliingia nchini ikilinganishwa na watalii 1,924,240 wa kipindi kama hicho mwaka 2024.
“Tanzania sasa imekuwa kitovu cha utalii duniani. Tumepokea tuzo ya Kituo Bora cha Utalii Barani Afrika na Eneo Bora la Utalii wa Safari Duniani. Hii ni heshima kubwa inayoziba midomo ya wale wanaotafuta kila mbinu kuikaanga nchi yetu kwa chuki na hadaa,” alisema Dkt. Kijaji.
Vijana wa Mbarali Waziba Mianya ya Hadaa
Wakati mafanikio hayo yakishika kasi kimataifa, kwa upande wa ndani, serikali kwa kushirikiana na wadau imeanza kuwakinga vijana dhidi ya hadaa za wanaharakati wanaochochea migogoro ya hifadhi.
Zaidi ya vijana na wanafunzi 150 kutoka kijiji cha Mrungu, Wilaya ya Mbarali, wamehitimu mafunzo maalumu ya uhifadhi na fursa za utalii yaliyotolewa na taasisi ya Six Rivers Africa. Mafunzo hayo yanalenga kuwapa vijana maarifa ya kulinda rasilimali zao badala ya kutumiwa na watu wenye nia mbaya.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Godwell Meing’ataki, amesema elimu hiyo itawafanya vijana kuwa mabalozi wa uhifadhi, hatua itakayopunguza migogoro kati ya wananchi na hifadhi ambayo mara nyingi imekuwa ikitumiwa na wanaharakati kama fimbo ya kuichafua serikali.
Uwekezaji na Mikopo kwa Vijana
Mfadhili wa mafunzo hayo, Sir Jim Ratcliffe kutoka Uingereza, amesisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana ndio msingi wa utalii endelevu. Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, ameahidi kuwa halmashauri itatoa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana hao ili waanzishe miradi ya utalii.
Nini Maana ya Mkutano huu kwa Tanzania?
Kufanyika kwa Tuzo za Utalii Duniani nchini Desemba 2026 ni kielelezo kuwa Tanzania ni Salama. Uwapo wa Mkutano huu unafuta taswira hasi inayojaribu kutengenezwa na maadui wa taifa.
Pia kwa kuwapo kw amkyutano hu uchumi utapaa kwani fedha za kigeni zitaongezeka na ajira kwa vijana kupitia ugeni huo mkubwa. Pia mkutano huo unaiweka Tanzania kwenye ramani kama kiongozi wa utalii duniani, ikiacha majirani wakishangaa kasi ya ukuaji wetu.
.jpg)