
Hatua hiyo ni kielelezo tosha cha imani kubwa ambayo mataifa ya nje na washirika wa maendeleo wanayo kwa uongozi wa Rais Samia katika kuimarisha sekta za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wilayani Longido mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Losirwa, Balozi wa India nchini, Bishwadip Dey, alisema kati ya fedha hizo, Dola milioni 600 (Shilingi Bilioni 1.4) tayari zimeshatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya afya, elimu, maji na barabara.
Balozi Dey alisisitiza kuwa India haitoi fedha hizo kama wahisani tu, bali kama washirika wanaounga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa wananchi wake.
"Serikali ya India imetenga fedha hizi kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya. Sikuja Longido kama mtalii, nimekuja kama mwanafamilia kukagua miradi yetu," alisema Balozi huyo.
Katika ziara hiyo, Balozi Dey alizindua mradi wa maji wa Chemchemi ya Tono uliogharimu Shilingi Milioni 125, mradi utakaonufaisha zaidi ya watu 2,000. Aidha, alipongeza Kampuni ya Dar Solution kwa kutoa vifaa vya TEHAMA vya Shilingi Milioni 15 na kuchangia Shilingi Milioni 30 katika ujenzi wa shule shikizi.
Balozi aliahidi kuwa India itaendelea kufanyia kazi changamoto za elimu wilayani humo ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Naye Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido, Dkt. Steven Kiruswa, alimshukuru Balozi huyo na kueleza kuwa ushirikiano huo ni matokeo ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Rais Samia. Alisema nguvu za wananchi na wadau wa India zimesaidia kufikisha mabomba na matanki ya maji katika vitongoji vya Kisambi na Olomuki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salumu Kally, aliwataka wananchi kuitunza miradi hiyo kama mboni ya jicho ili kuwajengea imani wahisani waweze kuleta miradi mingi zaidi.