Manispaa ya Shinyanga imeshika nafasi
ya kwanza Kimkoa kati ya halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga Matokeo
ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba (PSLE) mwaka 2025, kwa kupata asilimia 87 ya ufaulu wa jumla hatua
ambayo inafanya kuendelea kung’ara.
Akizungumza na walimu katika hafla
ya kukabidhi tuzo kwa shule zilizofanya vizuri zikiwemo za serikali na binafsi,
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius
Mtatiro, amewapongeza walimu pamoja na Idara ya Elimu ya Awali na Msingi
kwa ubunifu wa kutoa motisha kwa walimu
wanaofanya vizuri.
Ameeleza kuwa walimu wanapaswa kujifunza kutoka shule zilizofanya vizuri
zaidi na kubadilishana uzoefu na mbinu bora za ufundishaji ili kuimarisha
ubunifu na ubora wa elimu Hatua hiyo itasaidia kuinua zaidi viwango vya elimu
ndani ya Manispaa ya Shinyanga.
Mafanikio hayo yameitambulisha
Manispaa hiyo kama kinara wa ubora wa elimu ya msingi, yakionesha dhamira
thabiti ya kuinua viwango vya elimu kwa vitendo,kupitia shule za serikali na
shule binafsi.
Kufuatia matokeo mazuri, idara ya Elimu ya Awali na Msingi Manispaa ya Shinyanga imeandaa hafla maalum ya kutunuku vyeti vya pongezi
kwa walimu pamoja na shule za msingi zilizofanya vizuri Mtihani wa Darasa la
Saba (PSLE) 2025 na Mtihani wa Upimaji wa Darasa la Nne (SFNA) 2025
Hatua hiyo imelenga kutambua mchango wa walimu na kuhamasisha juhudi zaidi katika kuinua taaluma ili kuleta tija zaidi
Kazi ya kukabidhi tuzo inaendelea kwa shule mbalimbali binafsi na za serikali
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Revocatus Lutunda
Hatua hiyo imelenga kutambua mchango
wa walimu na kuhamasisha juhudi zaidi katika kuinua taaluma ili kuleta tija
zaidi.
Akitoa taarifa ya matokeo hayo, Mkuu
wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi Manispaa ya Shinyanga, Mary Samson Maka, amesema mafanikio
hayo yametokana na ushirikiano wa
karibu kati ya walimu, wanafunzi, wazazi na wasimamizi wa elimu.
Amesema mshikamano huo umewezesha kuwepo kwa mazingira
bora ya kujifunzia na kufundishia, hali iliyochangia ufaulu mkubwa.
Amesema Manispaa ya Shinyanga pia
imeibuka ya kwanza kimkoa katika
Mtihani wa Upimaji Darasa la Nne (SFNA) kwa kupata asilimia 82.25 ya ufaulu wa jumla matokeo
hayo yanaonesha msingi imara wa elimu ya awali na mwelekeo chanya wa maendeleo
ya elimu ya msingi kuanzia ngazi za chini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Revocatus Lutunda, amesema walimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya elimu na taifa kwa ujumla.
Amepongeza bidii na moyo wa kujituma
wa walimu, akibainisha kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho kuwa uwekezaji katika elimu una matokeo chanya ya
muda mrefu.





