.jpg)
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito mzito kwa waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu nchini, kuitumia msimu huu wa kipekee wa ibada kuliombea Taifa amani, umoja, mshikamano na ustawi wa kijamii.
Katika hali ya kipekee ambapo kalenda za kidini zimekutana, Rais Samia Februari 18, 2026, ametuma salamu za heri na baraka kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, akisisitiza umuhimu wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu na kuimarisha uhusiano wa kibinadamu kupitia sala na sadaka.
Kwa upande wa waumini wa Kikristo wanaoanza safari ya siku 40 ya Kwaresma , Rais Samia amewatakia mfungo mwema wenye baraka, akiwataka kutumia ibada ya Jumatano ya Majivu kama fursa ya kutafakari na kuimarisha imani yao.
“Safari hii muhimu kiimani kwenu mnayoianza leo... iwe fursa ya kutafakari, kuendelea kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu; na kudumu katika ibada, kuiombea nchi yetu amani, umoja, mshikamano na ustawi kwa wote,” aliandika Rais Samia.
Rais alihitimisha salamu hizo kwa kunukuu Maandiko Matakatifu kutoka kitabu cha Yoeli 2:12-13, kinachosisitiza kurejea kwa Bwana kwa mioyo yote kupitia kufunga na kuomboleza, huku akisisitiza waumini "kurarua mioyo yao na si mavazi yao."
Wakati huo huo, Rais Samia amewatakia kheri na mfungo mwema Waislamu wote nchini wanapojiandaa au kuanza kutekeleza nguzo muhimu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Amewasihi waumini hao kusujudu kwa shukrani kwa neema ya kufikia mwezi huo adhimu.
“Tunapotekeleza nguzo hii muhimu, tumwombe (Mwenyezi Mungu) atujalie kudumu katika ibada na upendo kwake na jamii na akaipokee funga yetu,” alieleza Rais katika ujumbe wake.
Aliwakumbusha Waislamu wajibu wao wa kisheria na kiimani kwa kunukuu aya ya Qur’an Tukufu kutoka Sura Al-Baqara 183, inayosema: “Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.”
Rais Samia amehimiza kuwa katika vipindi hivi vya kufunga na kusujudu, waumini wa dini zote wasichoke kuiombea nchi ya Tanzania ili iendelee kubaki katika misingi ya amani na utulivu. Amewaombea wafungaji wote nchini ili Mwenyezi Mungu azipokee funga, sala na sadaka zao, na kuwakirimia mema kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia hadi Taifa kwa ujumla.
Tukio hili la dini zote mbili kubwa nchini kuingia katika kipindi cha toba na kufunga kwa wakati mmoja, limeonekana kama ishara ya kiroho ya kuimarisha umoja wa kitaifa, huku kauli ya Rais ikiongeza chachu ya utulivu na uchamungu nchi nzima.