WAKUU WA SHULE,WALIMU WAKUU KUWEKEANA MIKATABA NA WALIMU WAO KUONGEZA UFAULU KUFIKIA ASILIMIA 85


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, ameongoza zoezi la utoaji tuzo kwa shule zilizofanya vizuri kitaaluma mkoani humo 2025, ambapo pia ametoa maelekezo  kwa shule zilizofanya vibaya kuongeza juhudi na ubunifu ili kuinua viwango vya ufaulu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amesisitiza suala la kuongeza ufaulu mashuleni kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanafunzi kuongeza ufaulu kwani serikali imeweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Akizungumza katika kikao  kazi cha tathimini  ya utekelezaji wa shughuli za elimu Mkoani Shinyanga katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari ya wasichana Shinyanga,Mkuu wa Mkoa Mhita amewataka walimu kuongeza bidii na uwajibikaji katika kazi zao,huku akiwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya kuongeza ufaulu.

Amesema mafanikio ya elimu ni msingi wa maendeleo ya Mkoa na taifa kwa ujumla na kusisitiza kuwa mchango wa mwalimu una nafasi kubwa katika kuinua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi ambapo amewaagiza wakuu wa shule,walimu wakuu kuwekeana mikataba na walimu wao kuongeza ufaulu kufikia asilimia 85.

Katika hatua nyingine,Mkuu  wa Mkoa alielekeza shule zote kuhakikisha zinatoa chakula shuleni, akibainisha kuwa mpango huo utasaidia kuwaepusha wanafunzi na njaa, jambo linalochangia utoro na kushuka kwa kiwango cha uelewa darasani.

Alisema lishe bora shuleni ni nyenzo muhimu ya kuboresha mahudhurio na matokeo mazuri,ambapo  pia amesisitiza kuondolewa kabisa kwa tatizo la utoro wa wanafunzi kuhakikisha kila mwanafunzi anahudhuria masomo kikamilifu.

Katika kikao hicho tuzo zilitolewa kwa shule zilizofanya vizuri hatua iliyolenga kutambua na kuhamasisha juhudi za walimu na ni  motisha muhimu katika kuongeza ushindani chanya mashuleni.

Kwa shule ambazo hazikufanya vizuri, Mkuu wa Mkoa aliwataka kujitathmini kwa kina, kubaini changamoto zinazowakabili na kuchukua hatua za haraka za mabadiliko. Alisisitiza kuwa lengo si kulaumu bali kuboresha na kuhakikisha kila shule inapiga hatua.

Katika hatua nyingine Mhita ameagiza watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa kuanza darasa la kwanza kwa wakati,kwani ni haki ya mtoto kupata elimu ya msingi na ni wajibu wa jamii nzima.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye hafla hiyo ya kutunuku Tuzo
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi akizungumza.
Mkuu wa wilaya Kahama Frank Nkinda akizungumza.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akizungumza.
Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Samson Hango akizungumza.

Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Samson Hango akisoma taarifa ya hali ya elimu, amesema kiwango cha ufaulu kimeongezeka mkoani humo ikilinganishwa na mwaka jana.

Baadhi ya wakuu wa shule zilizopata tuzo wamesema mafanikio yao yametokana na utoaji wa chakula shuleni, ushirikiano mzuri kati ya wazazi na walimu, kufanya mitihani ya mara kwa mara, kudhibiti utoro na kutoa motisha kwa walimu. 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.

Muonekano wa Tuzo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akitoa Tuzo kwa shule ambazo zimefanya vibaya.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akitunuku Tuzo kwa shule ambazo zimefanya vizuri kitaaluma.

 

Post a Comment