
Jumla ya wananchi 63,541 mkoani Shinyanga wanatarajia kunufaika na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu kwa uhakika.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, wakati akifungua kikao cha Kamati
ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa, Shinyanga.
Amesema
utekelezaji wa mpango huo unaenda sanjari na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
“Lengo
letu ni kuona kila mwananchi anakuwa na uhakika wa kupata matibabu anapougua.
Hii ni hatua muhimu katika kuboresha ustawi wa jamii,” amesisitiza.
Katika hatua
nyingine, Mkuu wa Mkoa amesema suala la utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana
na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia kumi ya halmashauri linaendelea
kutekelezwa kwa mujibu wa miongozo ya Serikali.
Ameeleza kuwa mikopo hiyo inalenga
kuwawezesha makundi hayo kiuchumi ili kuongeza kipato chao na kuchangia
maendeleo ya mkoa.
Aidha, amepongeza
juhudi zinazoendelea katika kuboresha huduma za maji mijini na vijijini,
akieleza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama umeimarika kwa kiwango
kikubwa. Amesema Serikali itaendelea kusimamia miradi ya maji ili kuhakikisha
wananchi wote wanapata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo na afya zao.
Kikao hicho cha RCC kilijadili masuala mbalimbali ya
maendeleo, ikiwamo tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi,
kwa lengo la kuharakisha maendeleo endelevu katika Mkoa wa Shinyanga