Zoezi la
utoaji chanjo ya matone ya polio limeanza rasmi katika Mkoa wa Shinyanga, huku Serikali ikiweka
mkazo kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa kinga dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Wazazi na walezi wametakiwa kujitokeza kwa wingi
kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka kumi wanapatiwa chanjo hiyo
muhimu, inayolenga kulinda afya na mustakabali wa kizazi kijacho.
Uzinduzi huo
umefanyika katika Shule ya Msingi Mapinduzi B, Katibu Tawala wa Mkoa, Salum Hamdun, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa,
alisema jumla ya watoto 781,186 wanatarajiwa kufikiwa katika halmashauri zote
za mkoa huo.
Amesema zoezi hilo litatekelezwa kwa njia ya
nyumba kwa nyumba, mashuleni pamoja na katika vituo vya afya ili kurahisisha
upatikanaji wa huduma kwa watoto wote waliolengwa.
“Chanjo hii ni muhimu kwa watoto wetu, na yeyote atakayejaribu kukwamisha zoezi hili hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa lengo ni kuwafikia watoto wote
waliopo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo bila kuacha hata mmoja.
Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dinah Atinda, aliwapongeza wazazi kwa mwitikio wao, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na wataalamu wa afya ili kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya
Shinyanga, Salum Kitumbo, aliwahakikishia
wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama, akiwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao
wanapata huduma hiyo kwa wakati.
Alisema manispaa hiyo, kwa kushirikiana na wadau wa afya, imejipanga kikamilifu kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.




















































