MEGAWATI 50 ZA UMEME WA JUA KISHAPU ZAINGIA RASMI KWENYE GRIDI YA TAIFA

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao wametembelea  mradi wa kuzalisha umeme jua   pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli

 

Na Stella Herman,Shinyanga

Serikali imeendelea kupanua vyanzo vya uzalishaji wa umeme nchini kwa kutekeleza mradi wa umeme wa jua wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo awamu ya kwanza tayari imekamilika na kuanza kuzalisha megawati 50 zilizoingizwa kwenye gridi ya taifa.

 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo imefanya ziara katika eneo la mradi huo pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli kilichopo Manispaa ya Shinyanga imeridhishwa na miradi hiyo na kulipongeza Shirika la Tanesco kwa kazi nzuri.

Akizungumza leo Machi 13, 2026 wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgalu, amesema kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.

Mgalu ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya Nishati, akisema megawati 50 zilizozalishwa tayari zimeanza kunufaisha wananchi kupitia gridi ya taifa.

“Tunaipongeza serikali kwa utekelezaji wa mradi huu wa umeme wa jua. Tunafarijika kuona megawati hizi 50 tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa,” amesema Mgalu.

Ameishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo ambayo inatarajiwa kuzalisha megawati 100 ili kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.

Katika ziara hiyo, kamati pia ilitembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli ambapo Mgalu aliipongeza serikali kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi bilioni 207 kupanua kituo hicho.


Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akizungumza.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi amesema mradi wa umeme wa jua wa Kishapu ulianza kutekelezwa mwaka 2023 na awamu ya kwanza sasa imekamilika kwa kuzalisha megawati 50.

Alieleza kuwa ujenzi wa awamu hiyo umegharimu shilingi bilioni 118, huku serikali ikiendelea na maandalizi ya kuanza awamu ya pili.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Nishati na Madini Subira Mgalu akizungumza.








Post a Comment