Wananchi wametakiwa kutumia Nishati safi ya kupikia ili kuepuka kukata miti hovyo kwa ajili ya kuni na mkaa na kusababisha uharibifu wa misitu na mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya
Shinyanga, Said Kitinga, ambaye amemwakilisha
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, akizungumza leo Machi
20,2026 wakati wa kupanda miti shule ya sekondari ya wasichana Shinyanga ikiwa
ni kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Machi 21 amesisitiza umuhimu wa
kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kulinda mazingira.
Amesema Wakala wa
misitu Tanzania (TFS) wanafanya kazi kubwa katika kuhakikisha misitu inaendelea
kuwa salama ili kulinda mazingira yasiharibiwe na shughuli za kibinadamu.
Amesema ushirikiano kati ya shule ya sekondari ya
wasichana Shinyanga na (TFS), ambao leo Machi 20, 2026, wameshiriki
kupanda miti 350 shuleni hapo yameleta mafanikio makubwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani
yanayofanyika kila Machi 21.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda ya Magharibi, Shadrack Msilu, amesema lengo la kupanda miti katika shule hiyo ni kutoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Amesema hatua hiyo pia inalenga kuhamasisha wananchi kuacha tabia ya ukataji miti holela na badala yake kujikita katika upandaji miti kama njia ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
“ Takribani hekta 406,900 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu, hali inayotishia mustakabali wa mazingira yetu,” amesema Msilu.
Mwenyekiti wa Klabu ya Mazingira ya shule hiyo, Kabula Bundala, amesema tangu kuanzishwa kwa
klabu hiyo mwaka 2023, shule ilikuwa na mti mmoja tu wa asili, lakini kupitia
juhudi za pamoja na TFS, wamefanikiwa kupanda miti mingi hadi kufikia jumla ya
miti 12,053.
Amesema klabu hiyo imekuwa chachu ya
mabadiliko kwa wanafunzi, ikiwawezesha kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa
mazingira na kujenga utamaduni wa kupanda na kutunza miti.
Hatua hiyo inaonesha namna taasisi za elimu zinavyoweza kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto za mazingira kwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya kijani inayohusisha wanafunzi moja kwa moja.