VIONGOZI WATOA UJUMBE MZITO WAKATI WA FUTARI YA TAKUKURU:RUSHWA HAINA NAFASI

Baadhi ya wafanyakazi wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga
wakiwa na viongozi wa dini,chama na serikali
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Sunday Mtatiro,akizungumza na wananchi katika iftar ya jion .


Akihimiza umuhimu wa uwajibikaji na uadilifu katika jamii, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Sunday Mtatiro, amewataka wananchi kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kuimarisha haki na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Amesema rushwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo na husababisha upotevu wa rasilimali za taifa, huku akibainisha kuwa vitendo hivyo vinahusisha pande zote mbili—wanaotoa na wanaopokea.
“Mapambano ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinasimamiwa kwa uadilifu na kunufaisha wote,” amesema Mtatiro.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Shinyanga imeandaa futari maalum kwa waumini wa dini ya Kiislamu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kukuza ushirikiano katika vita dhidi ya rushwa.

Hafla hiyo iliyofanyika katika hali ya utulivu na upendo imewakutanisha viongozi wa dini, serikali pamoja na wananchi wa kada mbalimbali, ambapo pia ilitumika kama jukwaa la kuwaunganisha pamoja.

Akizungumza katika futari hiyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kuwa karibu na jamii si tu katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria, bali pia kushiriki katika matukio ya kijamii yanayokuza umoja na mshikamano.

Alieleza kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi, akiwahimiza kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya vitendo vya rushwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
Kwa upande wao, viongozi wa dini ya Kiislamu wameishukuru TAKUKURU kwa kuandaa futari hiyo, wakisema imekuwa fursa muhimu ya kuwakutanisha watu wa makundi mbalimbali na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya taasisi hiyo na jamii.

Wamesisitiza kuwa mshikamano unaojengwa kupitia matukio kama hayo ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo na kudumisha maadili mema, ikiwemo kupinga vitendo vya rushwa vinavyokwamisha ustawi wa jamii.

Futari hiyo imeacha ujumbe mzito kwa jamii kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja, huku mshikamano wa wananchi ukitajwa kuwa silaha muhimu katika kuhakikisha haki na maendeleo vinapatikana kwa wote.
 Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga ,Donnasian Kessy akizungumza katika iftar ya jioni machi,18,2026











Post a Comment