WADAU WA MAJI SHINYANGA WAJADILI NA KUSHAURI RASMU YA MKATABA WA HUDUMA KWA MTEJA

Mkutano wa wadau wa maji safi SHUWASA
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro

Na Stella Herman,Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, ametoa wito kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) kuhakikisha wanazingatia kikamilifu mkataba wa huduma kwa wateja pamoja na miongozo ya kisheria ili kuboresha utoaji wa huduma ya maji na kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maji uliofanyika leo Machi 26, 2026, Mtatiro amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, huku akitaka kero zinazowakabili watumiaji wa maji kutatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Katika mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kujadili rasimu ya mkataba mpya wa huduma kwa mteja, wametoa maoni mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma. Miongoni mwao, Ashirafu Said amependekeza kuanzishwa kwa mita za malipo ya kabla ili kupunguza malalamiko ya bili kubwa za maji.

Amesema kuwa ingawa kuna jitihada zinazoendelea za kuboresha huduma, bado mfumo wa sasa unasababisha malalamiko kwa baadhi ya wateja, hivyo matumizi ya mita za aina ya tokeni kama ilivyo kwa umeme yanaweza kuwa suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SHUWASA, Yusuph Katopola, ameeleza kuwa mkataba wa zamani umeisha muda wake, na mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha rasimu ya mkataba mpya utakaodumu kwa miaka mitatu kuanzia 2026 hadi 2029, baada ya kupitishwa na EWURA.

Amefafanua kuwa mkataba huo unaweka wazi haki na wajibu wa pande zote yaani mtoa huduma na mteja kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuimarisha mahusiano.

Kuhusu suala la mita za malipo ya kabla, Katopola amebainisha kuwa utekelezaji wake utafanyika kwa awamu kutokana na gharama zake kuwa kubwa, na zoezi hilo litaanza katika maeneo yenye changamoto za ulipaji, hususan vituo vya umma vya kuchotea maji, likitarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka huu.

Aidha, Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa SHUWASA, Rueben Mwandumbya, amewasilisha majukumu ya mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa maji safi na salama kwa viwango vinavyokubalika, kuboresha usafi wa mazingira, kujenga uhusiano mzuri na wateja, pamoja na kushughulikia malalamiko yao.

Ametaja pia haki za mamlaka kama kulipwa kwa huduma wanazotoa, pamoja na kusitisha huduma kwa wateja wasiolipa kwa wakati, na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu wa miundombinu au wezi wa maji.
Kwa upande wa wateja, walikumbushwa wajibu wao wa kulipa bili kwa wakati, kutoa ushirikiano kwa watumishi wa mamlaka, kulinda vyanzo vya maji, na kutoa taarifa sahihi kuhusu vitendo vya uharibifu au wizi wa maji.


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Mkurugenzi wa Shuwasa Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza.
Mkurugenzi wa huduma kwa wateja kutoka SHUWASA Rueben Mwandumbya akiwasilisha mkataba wa huduma kwa wateja.
Mwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Ruben Kitinya akizungumza.



M



Post a Comment