
Afisa Programu wa mpango wataifa wa chanjo Michael Ndowa.
Na Editha Edward,Geita
Watoto zaidi ya milioni moja wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa polio mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omari Sukari, alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya kugundulika kwa vimelea vya ugonjwa wa polio kwenye maji taka katika mkoa wa Mwanza.
Dkt. Sukari amesema kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuanza rasmi Machi 24 hadi 27 kwa awamu ya kwanza, ambapo wahudumu wa afya watawafikia wananchi moja kwa moja majumbani, stendi, masokoni pamoja na maeneo ya shule ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa.
Kwa upande wake, Afisa Programu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Michael Ndowa, aliwataka wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi ili watoto wao waweze kupata chanjo ya polio.
Alisema kuwa wamejipanga kufikia mikoa saba ambayo ni Mwanza, Mara, Geita, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Singida.

Aidha, alibainisha kuwa ni kawaida kwa Wizara ya Afya kufanya kampeni za chanjo hizo ili kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa wa polio.
