CHEREHANI AWASHUKURU WANANCHI USHETU: DARAJA LA MWABOMBA LAANZA KUTUMIKA, KITUO CHA AFYA IDAHINA KUJENGWA

 Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani akikaribishwa katika kijiji cha Mwabomba kata ya Idahina Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga. - Picha na Kadama Malunde  Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mwabomba Kata ya Idahina Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga 



Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani amefanya ziara muhimu ya kukagua na kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Idahina, Halmashauri ya Ushetu, sambamba na kufanya mkutano mkubwa wa shukrani kwa wananchi waliomchagua kuwa mbunge wao.

Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Jumatatu Aprili 13, 2026 Mhe. Cherehani ametembelea Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Mwabomba uliokamilika kwa asilimia 99 na tayari kuanza kutumika, pamoja na kuzindua rasmi ujenzi wa Kituo cha Afya Mwabomba (Idahina), hatua inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mwabomba, Mhe. Cherehani ametoa shukrani zake kwa wananchi pamoja na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu.
“Leo Aprili 13, 2026 ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima sote wananchi wa Ushetu. Nimekuja kusherehekea nanyi na kusema neno moja tu  ‘Asante’. Asanteni sana kwa kunichagua kuwa Mbunge wenu na kwa kumchagua Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais na madiwani wa CCM” amesema Cherehani.

Mbunge huyo ameeleza kuwa serikali imetoa shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mwabomba, ambalo sasa limeanza kuwahudumia wananchi bila hofu, huku akitangaza kukabidhi shilingi milioni 657 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Idahina.

“Nimekuja kuwakabidhi kiasi cha shilingi milioni 657 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na wananchi wasichangishwe hata shilingi mia. Tayari milioni 250 zipo kwenye akaunti, nataka ujenzi uanze mara moja ili wananchi waanze kupata huduma,” amesisitiza.

Aidha, ametoa maagizo kwa watendaji wa sekta ya afya kuhakikisha huduma kwa wajawazito zinatolewa bila malipo, akipiga marufuku vitendo vya kuwatoza fedha.

“Ni marufuku kumtoza hata shilingi 10 mama mjamzito. Wapokeeni, wapimeni na wahudumieni. Hawa ni wananchi wa kawaida, wanashinda mashambani ,wanatoa wapi fedha?” amehoji.
Mbali na afya, Mhe. Cherehani amezungumzia mipango ya maendeleo ikiwemo upatikanaji wa maji kupitia mradi wa Ziwa Victoria, ufunguzi wa soko la dhahabu Mwabomba na utatuzi wa changamoto za wafugaji kupata maeneo ya malisho.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa aliyekuwa mgeni rasmi amempongeza Mhe. Cherehani kwa kusimamia kwa vitendo miradi ya maendeleo.
“Ushetu mna mbunge mchapakazi, mmelamba dume sana, ni mbunge wa Vitendo, Cherehani inashona maendeleo kweli kweli Ushetu. Ni vigumu kupata kiongozi mwenye upendo na jitihada kama hizi. Daraja la Mwabomba sasa linapitika, wananchi wanavuka bila hofu,” amesema Mlolwa.

Ameongeza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na maono ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, huku akihimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kuunga mkono serikali yao ili kuharakisha maendeleo zaidi.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na kudumisha amani, akibainisha kuwa maendeleo yanayoonekana ni matokeo ya sera na utekelezaji wa CCM chini ya uongozi wa Rais Samia.

Mradi wa Daraja la Mwabomba kwenye barabara ya Masumbwe–Mwabomba unaounganisha mikoa ya Shinyanga na Geita, umetekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na mkandarasi M/s Jossam & Co. Ltd, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kufuatia uharibifu wa miundombinu uliotokea hapo awali.

Post a Comment