
Na Stella Herman, Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro amesema hakuna nafasi ya visingizio pale dharura zinapotokea hasa katika kipindi hiki cha masika ili kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya miundombinu ya barabara.
Mtatiro ametoa kauli hiyo usiku
alipofika kukagua utekelezaji wa maagizo ya serikali katika eneo korofi la
barabara ya Didia–Solwa upande wa Kata ya Ilola,ambapo amesisitiza kuwa hatua
za haraka zimechukuliwa ili kuhakikisha
wananchi wanapita bila usumbufu.
“Nimefika hapa usiku huu kufuatilia
utekelezaji wa maagizo ya serikali kuhakikisha barabara hii inakamilika haraka
na namshukuru sana Mhe diwani Kisena kwa kusimamia suala hili” amesema
Ameonya kuwa si jambo linalokubalika
kwa miundombinu iliyopata dharura kusubiri kwa muda mrefu kupata bajeti, amesema
hatua za dharura zinapaswa kuchukuliwa mapema ili kuzuia madhara makubwa zaidi.
Mtatiro amebainisha kuwa kipande cha
barabara chenye urefu wa kilomita mbili kilikuwa katika hali mbaya na kingeweza
kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya maeneo ya Solwa na Didia endapo
hatua za haraka zisingechukuliwa.
Amempongeza Diwani wa Kata ya Ilola,
Kisena, kwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu changamoto hiyo, akieleza kuwa
hatua hiyo imewezesha serikali kuingilia kati kwa haraka na kuwanusuru wananchi
na wafanyabiashara waliokuwa hatarini kushindwa kupitisha mazao yao.
Aidha, alimuelekeza mkandarasi
anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi inakamilika ifikapo Aprili 10, 2026
ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwa wananchi.
Meneja wa TARURA Mhandisi Samson pamphil amesema barabara ya Didia–Solwa yenye urefu wa kilomita 55.3 ilikuwa imeharibika vibaya kufuatia mvua za masika hali iliyosababisha kutokea kwa madimbwi makubwa na mashimo yaliyokuwa yanahatarisha usalama wa watumiaji.

Kutokana na hali hiyo, wananchi walikuwa wakipata ugumu wa kupita, huku baadhi ya wanafunzi wakishindwa kupita hadi wapate msaada wa kuwavusha kama ilivyotokea kwa diwani wa Kata ya Ilola Kisena Fred ambaye wakati imetokea changamoto hiyo alikutana na watoto na kuwavusha kwa kutumia pikipiki.
Changamoto hiyo ilibainika Februari 19, 2026, na baada ya kuripotiwa kwa mamlaka husika, hatua za haraka zilichukuliwa ikiwemo kumtumia mkandarasi aliyekuwa akifanya kazi Kata ya Lyabukande kushughulikia eneo hilo lililokuwa na uhitaji wa dharura.
Wananchi wa Kata ya Ilola wameishukuru serikali ya Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua za haraka kurekebisha barabara hiyo, wakisema imekuwa mkombozi mkubwa kwao na imeondoa adha waliokuwa wakikabiliana nayo kwa muda.
“Kweli serikali ya Mama Samia imesikia kilio chetu, hatua zimechukuliwa haraka na sasa tunaanza kuona matokeo,” walisema baadhi ya wananchi.
.jpeg)




.jpeg)