WAJAWAZITO BUSANGI WALALAMIKIA TOZO ZISIZO RASMI KLINIKI NA FAINI WAKIJIFUNGULIA NYUMBANI

       Na Mwandishi wetu,Shinyanga

Katika hali inayozua maswali juu ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa  wajawazito, wanawake  Kata ya Busangi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, wametoa kilio chao  kutozwa fedha zisizo rasmi wanapohudhuria kliniki pamoja na kutozwa faini wanapojifungulia nyumbani au njiani.

Malalamiko hayo yametolewa na wanawake hao  katika mkutano wa hadhara  ulioitishwa na Mbunge wa Jimbo la Msalala Mabula Magangila, ambapo  wameeleza changamoto wanazokumbana nazo wanapotafuta huduma za afya.

Kwa mujibu wa wananchi hao, mjamzito hulazimika kulipa shilingi elfu kumi na mbili anapoanza kliniki kwa mara ya kwanza katika Zahanati ya Busangi na kutozwa faini ya Shilingi elfu thelathini endapo watajifungulia nyumbani au njiani, jambo linaloongeza mzigo kwa familia nyingi zenye kipato cha chini.

Akizungumza katika mkutano huo mkazi wa Busangi Agnes Makenzi amesema hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwa wajawazito kupata huduma stahiki kwa wakati, na kuiomba serikali kuingilia kati ili kukomesha vitendo hivyo vinavyodaiwa kukiuka haki za msingi za afya.


Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge wa Jimbo la Msalala

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Busangi Prisca Joseph, alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kueleza kuwa tayari ameanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kumnusuru  mjamzito aliyeombwa fedha na kufanikiwa kumsaidia kuepuka kulipa kiasi hicho.

Wakati huo huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Msalala, Emmanuel Michael, ametoa onyo kali kwa watumishi wa afya wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Amesisitiza kuwa hakuna mwongozo wowote unaoruhusu kutozwa fedha kwa wajawazito wanapoanza kliniki au wanapojifungua.

Amesema kuwa vitendo hivyo ni kinyume na maadili ya kazi za afya na kuwataka wahusika kuacha mara moja, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia weledi na utu katika utoaji wa huduma.

Naye Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila amesikitishwa  na hali hiyo na kueleza  kuwa wananchi wanapaswa kupata huduma bora za afya bila vikwazo vyovyote huku  akitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika ili kukomesha kabisa vitendo hivyo.

 Ombi la wanawake wa Busangi sasa ni kuona serikali ikichukua hatua za haraka ili kulinda haki zao na kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto.





Post a Comment