
Na Mwandishi wetu,Shinyanga
Katika hali inayozua maswali juu ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wajawazito, wanawake Kata ya Busangi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, wametoa kilio chao kutozwa fedha zisizo rasmi wanapohudhuria kliniki pamoja na kutozwa faini wanapojifungulia nyumbani au njiani.
Malalamiko hayo yametolewa na
wanawake hao katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Jimbo la Msalala
Mabula Magangila, ambapo wameeleza
changamoto wanazokumbana nazo wanapotafuta huduma za afya.
Kwa mujibu wa wananchi hao, mjamzito
hulazimika kulipa shilingi elfu kumi na mbili anapoanza kliniki kwa mara ya kwanza
katika Zahanati ya Busangi na kutozwa faini ya Shilingi elfu thelathini endapo
watajifungulia nyumbani au njiani, jambo linaloongeza mzigo kwa familia nyingi
zenye kipato cha chini.
Akizungumza katika mkutano huo mkazi
wa Busangi Agnes Makenzi amesema hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwa
wajawazito kupata huduma stahiki kwa wakati, na kuiomba serikali kuingilia kati
ili kukomesha vitendo hivyo vinavyodaiwa kukiuka haki za msingi za afya.


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa
Zahanati ya Busangi Prisca Joseph, alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na
kueleza kuwa tayari ameanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kumnusuru mjamzito aliyeombwa fedha na kufanikiwa
kumsaidia kuepuka kulipa kiasi hicho.
Wakati huo huo, Kaimu Mganga Mkuu wa
Halmashauri ya Msalala, Emmanuel Michael, ametoa onyo kali kwa watumishi wa
afya wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Amesisitiza kuwa hakuna mwongozo
wowote unaoruhusu kutozwa fedha kwa wajawazito wanapoanza kliniki au
wanapojifungua.
Amesema kuwa vitendo hivyo ni
kinyume na maadili ya kazi za afya na kuwataka wahusika kuacha mara moja, huku
akisisitiza umuhimu wa kuzingatia weledi na utu katika utoaji wa huduma.

Naye Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula
Magangila amesikitishwa na hali hiyo na
kueleza kuwa wananchi wanapaswa kupata
huduma bora za afya bila vikwazo vyovyote huku
akitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika ili kukomesha kabisa
vitendo hivyo.
Ombi la wanawake wa Busangi sasa ni kuona
serikali ikichukua hatua za haraka ili kulinda haki zao na kuboresha huduma za
afya kwa mama na mtoto.







