
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano
na Amani Mkoa wa Shinyanga, Shekhe Balilusa Khamis, ameiomba serikali kutozipuuza kauli zinazotolewa na
baadhi ya watu, hususan viongozi wa kijamii na kisiasa, ambazo zinaweza
kuhatarisha usalama wa wananchi na utulivu wa taifa wachukuwe hatua kali.
Akizungumza katika mahojiano maalum katika
muktadha wa kuimarisha mshikamano wa kijamii, amesema kuna mwenendo
unaojitokeza wa baadhi ya watu kutoa maneno yasiyo na staha na yasiyo sahihi,
jambo ambalo linaweza kuchochea taharuki na migogoro isiyo ya lazima endapo
halitachukuliwa hatua mapema na kuhatarisha amani na utulivu.
Aonya Madhara ya Kauli za Uchochezi
Shekhe Khamis amesisitiza kuwa suala
la amani si la kubezwa, bali ni jukumu la msingi la serikali kulinda na
kuhakikisha linaendelea kudumu wakati wote. Ameonya kuwa mtu mmoja mwenye kauli
potofu anaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii, akieleza kuwa historia
imeonesha kuwa migogoro mingi huanzia kwenye maneno yasiyopimwa.
“Ni muhimu watu wakakemewa mapema,
Kauli zisizo na msingi zinaweza kuleta maafa makubwa, Serikali inapaswa kuwa
makini na kuchukua hatua dhidi ya upotoshaji unaoendelea,” amesisitiza Balilusa
Amesema Tume ya kuchunguza matukio
ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 imefanya kazi kubwa na
inahitaji kuungwa mkono kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yake ili kuchukuwa
hatua.
Vijana Wakumbushwa Kutambua Historia
ya Taifa
Katika nasaha zake kwa vijana,
Shekhe Khamis amewataka kutambua mabadiliko chanya yaliyopatikana nchini kwa
kulinganisha maisha ya sasa na ya zamani, Amesema vijana wanaolalamikia hali ya
maisha wanapaswa kuwauliza wazee wao ili kuelewa safari ya maendeleo iliyopatikana
ikilinganishwa na zamani.
Ameeleza kuwa tofauti na zamani
ambapo huduma muhimu kama umeme na miundombinu bora zilikuwa adimu, kwa sasa
kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, makazi na
huduma za kijamii.
Aidha, amekosoa tabia ya baadhi ya
watu kulinganisha maisha ya Tanzania na nchi nyingine bila kuzingatia mazingira
halisi ya kila taifa, amesema mtazamo huo unaweza kupotosha fikra za wananchi
na kuondoa ari ya kujivunia na kujenga nchi yao.
“Tunapaswa kujivunia tulichonacho na
kuendelea kukijenga. Kukimbilia kulinganisha na mataifa mengine ni hatari kwa
ustawi wa taifa letu,” amesema.
Amebainisha kuwa katika baadhi ya
nchi, migogoro imekuwa ikichochewa na kauli za wanasiasa wanaopotosha ukweli
ili kujijengea umaarufu, Hali hiyo, amesema, inaweza kujitokeza pia endapo
jamii haitakuwa makini na kuchambua taarifa wanazozipokea.
Kwa upande mwingine, amewasihi
vijana kujenga utamaduni wa kuchuja na kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichukua
kama ukweli. Amesema kukubali kila kinachosemwa bila uchunguzi kunaweza
kusababisha maamuzi yasiyo sahihi na hatimaye kuhatarisha amani ya nchi.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila Mtanzania, akiwataka wananchi wote kushirikiana na serikali katika kukemea vitendo na kauli zinazoweza kuvuruga utulivu uliopo.