
Timu ya Stand United imeingia katika mabadiliko mapya ya kiuongozi baada ya Mwenyekiti wake wa mpito, Issa Mbaraka, kutangaza kujiuzulu rasmi wadhifa huo kufuatia changamoto za ndani zilizokuwa zikiikumba timu hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari Mei
Mosi, 2026 mkoani Shinyanga, Mbaraka amesema uamuzi wake umetokana na tofauti
kubwa za kimtazamo kati yake na baadhi ya viongozi wenzake, hali iliyokuwa
ikiathiri ufanisi wa majukumu yake pamoja na maendeleo ya timu.
Ameeleza kuwa alichukua uamuzi huo
kwa nia njema ya kuinusuru Stand United, ili kutoa nafasi kwa wengine kuendelea
kuiongoza kwa mtazamo wanaouona unafaa zaidi.
Mbaraka amesema aliteuliwa kushika
nafasi hiyo mnamo Novemba 2025 na wadau wa timu, kwa lengo la kuirejesha katika
ushindani mzuri baada ya kuwa katika kipindi kigumu cha matokeo yasiyoridhisha.
Aidha, amebainisha kuwa licha ya
jitihada zake za kuiboresha timu na kuanza kupata matokeo chanya, bado
alikumbana na changamoto ya kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya
viongozi, jambo lililoathiri mwelekeo wa uongozi.
“Leo Mei Mosi, 2026 natangaza rasmi
kujiuzulu nafasi yangu na sitahusika tena na usimamizi wa timu ya Stand United,
kwa kuwa mtazamo wangu wa uongozi unatofautiana na viongozi wenzangu, hali
inayoniwekea vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yangu,” amesema Mbaraka.
Ameongeza kuwa aliona ni vyema
kuwaachia wengine waendelee na mfumo wao wa uendeshaji, huku yeye akilenga
kulinda heshima yake katika jamii kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea ndani
ya timu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga, Said ManKilingo, amesema amepokea taarifa
hizo kupitia vyombo vya habari na kumshauri Mbaraka kuwasilisha rasmi barua ya
kujiuzulu ili kukamilisha taratibu.
ManKilingo ameongeza kuwa kama
angepata nafasi ya kuzungumza naye kabla ya kufikia uamuzi huo, angeweza
kumshauri na kusaidia kutafuta suluhu ya changamoto zilizokuwa zikikabili
uongozi wa timu hiyo.
Naye Mjumbe wa mkutano mkuu TFF kutoka Mkoa wa
Shinyanga Azan Said Mufti amesema
kuisaidia timu ya Stand United ni kutokana na kila mtu alivyojaliwa na namna
ambavyo anapata msukumo kutoka ndani ya moyo wake na hakuna mtu anaye
lazimishwa isipokuwa ni kuipenda timu na kuisaidia ili ipige hatua huku
akibainisha kuwa hana taarifa za Mwenyekiti wa mpito wa timu hiyo kujiuzulu.