
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Stella Herman,Shinyanga
Kampeni ya kitaifa ya Samia Legal Aid inatarajiwa kuanza kutekelezwa mkoani Shinyanga kuanzia Mei 6 hadi Mei 20, 2026, ikiwa na lengo la kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu zaidi na wananchi na kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii.
Akizungumza na vyombo vya habari Mei 5, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema maandalizi ya kampeni hiyo yamekamilika, huku timu ya wataalamu wa sheria ikipangwa kufika katika kata zote 130 za mkoa huo ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma hiyo bila usumbufu.
Mhita ameeleza kuwa huu ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha haki inapatikana kwa wote, hasa kwa wale wasio na uwezo wa kugharamia huduma za kisheria.
Amesisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi pamoja na kuimarisha uelewa wa masuala ya sheria, akibainisha kuwa huduma zitatolewa moja kwa moja katika maeneo yao ya makazi.
“Hii ni nafasi adhimu kwa wananchi kupata msaada wa kisheria bila gharama. Serikali imeweka mazingira rafiki kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na huduma hizi muhimu,” amesema Mhita.

Aidha, amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza iliyofanyika mwaka 2023, jumla ya migogoro 578 ilishughulikiwa ambapo 378 ilipatiwa ufumbuzi, huku zaidi ya wananchi 22,000 wakinufaika na huduma hiyo.
Kwa mwaka huu, kampeni itaendeshwa kwa muda wa wiki mbili na itahusisha utoaji wa ushauri wa kisheria, elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu, uandaaji wa nyaraka mbalimbali za kisheria pamoja na uwakilishi katika vyombo vya mahakama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kisheria Mkoa wa Shinyanga, John Shija, amesema matarajio ni makubwa katika awamu hii ya pili, akieleza kuwa juhudi zimefanyika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wa makundi yote bila ubaguzi.
Ametoa wito kwa wakazi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa hiyo, akisisitiza kuwa msaada huo unaweza kusaidia kutatua migogoro kwa njia halali na kudumisha amani katika jamii.
Katika utekelezaji wa kampeni hiyo, vituo maalum vitatumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo Shinyanga Manispaa (Nguzo Nane), Kishapu (Mhunze na Ukenyenge), Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Didia na Iselamagazi), Kahama (Isaka – eneo la Posta), pamoja na Ushetu (Nyamalangano na Msalala), ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.