Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga sasa hawatalazimika tena kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuwasilisha malalamiko, maoni, ushauri au kero zao, baada ya Serikali kutambulisha mfumo wa kidigitali utakaorahisisha upatikanaji wa huduma kwa haraka na wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ametambulisha mfumo huo leo Juni 17,2026 katika idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ikiwa ni jitihada za kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo
mkuu wa mkoa Mhita amesema mfumo huo
unalenga kuwapa wananchi fursa ya kuwasilisha malalamiko, kero, maoni na
mapendekezo yao kwa njia rahisi za kidigitali bila kujali walipo.
Amesema pamoja na viongozi wa
Serikali kuendelea kufanya ziara za kusikiliza na kutatua kero za wananchi
katika maeneo mbalimbali, mfumo huo utaongeza ufanisi kwa kuwa wananchi
wataweza kuwasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wowote bila kulazimika
kusafiri.
Mkuu wa mkoa amesema wananchi
wanaweza kutumia simu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa namba 0737 108 177,
jukwaa la WhatsApp, barua pepe rcshinyanga@go.tz, pamoja na mfumo wa E-Mrejesho
kuwasilisha taarifa zao.
Ameeleza kuwa mfumo wa E-Mrejesho
utawaruhusu wananchi kutoa maoni, kuuliza maswali, kuwasilisha malalamiko na
kupendekeza maboresho ya huduma mbalimbali za Serikali kwa urahisi na kwa
usalama.
Aidha, amesema mfumo huo una usiri wa taarifa za wananchi, hivyo mtoa taarifa anaweza kuwasilisha ujumbe wake bila kutambulika endapo atahitaji kufanya hivyo.
"Mwananchi
anaweza kupiga simu au kuwasilisha taarifa wakati wowote,masuala ya usalama na
maendeleo ya Taifa ni jukumu la kila mmoja wetu," amesema Mhita.
Kwa wananchi wasiokuwa na huduma ya
intaneti, Mkuu huyo wa Mkoa amesema wanaweza kutumia huduma ya USSD kwa
kupiga *152*00#, kisha kuchagua namba 03 na kufuata maelekezo
yatakayowawezesha kupata huduma.
Amesema kauli mbiu ya mpango huo ni "Sema
Usikike", ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga
kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kusikika na changamoto zake
kushughulikiwa kwa wakati.
Mhe. Mhita amesisitiza kuwa viongozi
wote pamoja na idara za Serikali mkoani Shinyanga zinawajibika kushughulikia
kwa haraka maoni, malalamiko na mapendekezo yatakayowasilishwa kupitia mfumo
huo, hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa
wananchi.