Wananchi wakipatiwa huduma kupitia ofisi inayotembea ya TRA katika mnada wa Tinde ikiwa ni hatua ya kusogeza huduma karibu kwa wananchi


Katika jitihada za kusogeza huduma karibu kwa wananchi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imeanza rasmi kutoa huduma kupitia ofisi inayotembea, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya walipakodi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma .
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo katika mnada wa Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga leo Juni 16,2026 Afisa wa Kodi wa TRA Mkoa wa Shinyanga Semeni Mbeshi amesema ofisi inayotembea imeanza rasmi kutoa huduma katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kuwafikia walipakodi moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara.
Amesema huduma hiyo itawawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za kikodi kwa urahisi, kupunguza gharama na muda wa kufuata huduma katika ofisi za TRA pamoja na kutoa fursa ya kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Kupitia ofisi inayotembea wananchi wamepatiwa huduma zote zinazotolewa na TRA huku akitoa rai kwa wengine kuchangamkia fursa hiyo .
Baadhi ya wafanyabiashara waliohudumiwa katika mnada wa Tinde wameipongeza TRA kwa kuanzisha huduma hiyo, wamesema imewarahisishia upatikanaji wa huduma na kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu.
Wameiomba TRA kuendelea kupeleka huduma ya ofisi inayotembea katika maeneo mengine ili walipakodi wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo, wakieleza kuwa hatua hiyo itachangia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na wananchi.
TRA inaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali kupitia ofisi inayotembea na kuwaomba kuchangamkia fursa hiyo.



