SI MEDIA

SI MEDIA

The list of favorite articles does not exist yet...

View all articles
  • Sitemap
  • Disclaimer
  • Privacy
Home
HABARI

WANANCHI WAVUTIWA NA ELIMU YA VIPIMO SAHIHI, WAAHIDI KUWA MABALOZI WA WMA

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, Dodoma, wameeleza kufurahishwa na elimu wanayoipata kuhusu matumizi sahihi ya vipimo na kuahidi kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhakiki vipimo katika shughuli za kila siku.
Siku ya tatu ya maonesho hayo yaliyofunguliwa Juni 16 na yanayotarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026, banda la WMA limeendelea kuvutia idadi kubwa ya wananchi wanaotaka kujifunza namna Serikali inavyohakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara na huduma mbalimbali vinakuwa sahihi na vya kuaminika.
Mmoja wa wananchi hao, Bw. Bilson Vedastus, alisema elimu aliyopata imemsaidia kuelewa mambo muhimu ya kuzingatia anaponunua mafuta, gesi ya kupikia na bidhaa nyingine zinazopimwa.
“Awali sikuwa naelewa mambo haya kwa kina, lakini sasa najua ninachopaswa kuangalia ninapojaza mafuta, kununua sukari au gesi ya kupikia,” alisema.
Kwa upande wake, Bi. Asha Siyaya alisema elimu hiyo imewapa uwezo wa kutambua udanganyifu unaoweza kufanywa kupitia vipimo visivyo sahihi na kuahidi kutoa taarifa pale watakapobaini ukiukwaji.
“Tumeona jinsi pampu za mafuta, mizani na vifaa vingine vinavyohakikiwa ili kuhakikisha vinapima kwa usahihi. Hatuwezi kukaa kimya tukiona mteja anadhulumiwa. Tutawaeleza wengine na kuripoti udanganyifu popote tutakapouona,” alisema.
Wataalamu wa WMA, Albogast Kajungu, Mbwana Amani na Said Ibrahim, waliwaeleza wananchi kuwa huduma za uhakiki wa vipimo zinagusa sekta nyingi zinazohusiana moja kwa moja na maisha ya kila siku ya wananchi.

Walifafanua kuwa pampu za mafuta huhakikiwa na kuwekewa alama za uthibitisho, huku mizani inayotumika sokoni na madukani kupimia bidhaa mbalimbali ikikaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha watumiaji wanapata kiwango stahiki cha bidhaa wanazonunua.

Aidha, mita za maji na umeme zinazotumika majumbani na katika biashara huhakikiwa ili kuhakikisha wateja wanalipia matumizi halisi, huku mitungi ya gesi ya kupikia, bidhaa zilizofungashwa pamoja na mizani za kupimia uzito wa magari barabarani nazo zikiendelea kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo, Bi. Veronica Simba, alisema lengo la WMA ni kuhakikisha kila mwananchi anapata thamani halisi ya fedha anayolipia bidhaa na huduma mbalimbali.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutembelea banda la WMA katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu haki zao na umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli za kijamii na kiuchumi.


WANANCHI WAVUTIWA NA ELIMU YA VIPIMO SAHIHI, WAAHIDI KUWA MABALOZI WA WMA

Post a Comment

TAFUTA HABARI

HABARI KALI WIKI HII

HATIBU  MGEJA MWENYEKITI MPYA TRCS MKOA WA SHINYANGA,ASISITIZA USHIRIKIANO KUKIJENGA CHAMA

HATIBU MGEJA MWENYEKITI MPYA TRCS MKOA WA SHINYANGA,ASISITIZA USHIRIKIANO KUKIJENGA CHAMA

Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) Mkoa wa Shinyanga kimefanya uchaguzi wa viongozi wapya, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uongozi …

BARRICK KUENDELEA KUNUFAISHA WATANZANIA KUPITIA UTEKELEZAJI WA SERA YA MAUDHUI YA NDANI

VICHWA VYA HABARI MAGAZETI YA LEO ALHAMISI JULAI 23,2026

WMA YAUNGANA NA RAIS DKT. SAMIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MASHUJAA DODOMA

CHUO CHA SAYANSI ZA AFYA KOLANDOTO KUONGEZA WATAALAMU WA AFYA WENYE WELEDI ,KUPANDISHWA HADHI KUWA CHUO KIKUU

VICHWA VYA HABARI MAGAZETI YA LEO JULAI 25, 2026

VICHWA VYA HABARI MAGAZETI YA LEO JULAI 22,2026

CHAGUA HABARI

Tunajenga Ufahamu Mpya