
Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga limesema uvunjifu wa amani uliotokea katika kijiji cha Idukilo wilaya ya Kishapu kutokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi zimesababisha uharibifu wa mali mbalimbali ikiwemo kuvunjwa kwa baadhi ya maduka ya wafanyabiashara.
Kufuatia matukio mawili yaliyotokea
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu 75 wanaotuhumiwa kuhusika
na matukio hayo ya uvunjifu wa amani,huku kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa
Shinyanga Janeth Magomi amesema hakuna kifo kilichotokea.
Akizungumza kuhusu matukio hayo leo Juni 5,2026 Kamanda Magomi, amesema vurugu hizo
zilifanywa na baadhi ya wananchi na kusababisha uharibifu wa mali mbalimbali,
huku akisisitiza kuwa jukumu la Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao.
Amesema wananchi hao wanadai hawamtaki diwani wa kata ya Idukilo na hawataki kuona shughuli za serikali zikifanyika katika kata hiyo ambapo hali hiyo imesababisha viongozi wote wa Kijiji cha Sanjo kujiuzulu kutokana na hali hiyo.
Amesema Juni 1, 2026 majira ya saa 6:30 usiku katika
Kijiji cha Idukilo, ambapo baadhi ya wananchi walishambuliwa kwa madai ya kuwa
walikuwa wakitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Wilaya kuhusu watu
wanaohusika na vitendo vya fujo katika eneo hilo.
Kamanda Magomi amesema
katika tukio jingine lililotokea Mei 28,2026 katika Kijiji cha Sanjo Kata ya Idukilo ambapo watumishi wa serikali walivamiwa na
kushambuliwa walipokuwa wakitekeleza zoezi la kuingiza kaya maskini katika
mpango wa TASAF.
Walioshambuliwa ni Mtendaji wa Kata
ya Idukilo, Masembe Msele (50), Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya
Mwaduiluhumbo, Rose Shao (38), Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo ambaye alikuwa
kaimu mtendaji wa kijiji pamoja na wajumbe watatu wa serikali ya kijiji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu
waliokuwa wakitumia pikipiki mbili waliwashambulia watumishi hao kwa vipigo
kabla ya kuchana nyaraka zilizokuwa zikitumika kuingiza majina ya baadhi ya
kaya maskini katika mpango wa TASAF. Washambuliaji hao walidai kuwa hawataki
kuona viongozi wa serikali wakifanya kazi ndani ya kata hiyo.
Baada ya matukio hayo mawili, Jeshi
la Polisi lilianzisha uchunguzi uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wanaodaiwa
kuhusika na vurugu, mashambulizi na uharibifu wa mali.