WATU 75 WANASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUPIGA WATUMISHI WA SERIKALI NA KUVUNJA MADUKA

Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga limesema uvunjifu wa amani uliotokea katika kijiji cha Idukilo wilaya ya Kishapu kutokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi zimesababisha uharibifu wa mali mbalimbali ikiwemo kuvunjwa kwa baadhi ya maduka ya wafanyabiashara.

Kufuatia matukio mawili yaliyotokea Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu 75 wanaotuhumiwa kuhusika na matukio hayo ya uvunjifu wa amani,huku kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amesema hakuna kifo kilichotokea.

Akizungumza kuhusu matukio hayo leo Juni 5,2026 Kamanda  Magomi, amesema vurugu hizo zilifanywa na baadhi ya wananchi na kusababisha uharibifu wa mali mbalimbali, huku akisisitiza kuwa jukumu la Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao.

Amesema wananchi hao wanadai hawamtaki diwani wa kata ya Idukilo  na hawataki kuona shughuli za serikali zikifanyika katika kata hiyo ambapo hali hiyo imesababisha viongozi wote wa Kijiji cha Sanjo kujiuzulu kutokana na hali hiyo.

 Amesema  Juni 1, 2026 majira ya saa 6:30 usiku katika Kijiji cha Idukilo, ambapo baadhi ya wananchi walishambuliwa kwa madai ya kuwa walikuwa wakitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Wilaya kuhusu watu wanaohusika na vitendo vya fujo katika eneo hilo.

Kamanda Magomi  amesema katika tukio jingine lililotokea Mei 28,2026 katika Kijiji cha Sanjo  Kata ya Idukilo  ambapo watumishi wa serikali walivamiwa na kushambuliwa walipokuwa wakitekeleza zoezi la kuingiza kaya maskini katika mpango wa TASAF.

Walioshambuliwa ni Mtendaji wa Kata ya Idukilo, Masembe Msele (50), Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Mwaduiluhumbo, Rose Shao (38), Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo ambaye alikuwa kaimu mtendaji wa kijiji pamoja na wajumbe watatu wa serikali ya kijiji.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu waliokuwa wakitumia pikipiki mbili waliwashambulia watumishi hao kwa vipigo kabla ya kuchana nyaraka zilizokuwa zikitumika kuingiza majina ya baadhi ya kaya maskini katika mpango wa TASAF. Washambuliaji hao walidai kuwa hawataki kuona viongozi wa serikali wakifanya kazi ndani ya kata hiyo.

Baada ya matukio hayo mawili, Jeshi la Polisi lilianzisha uchunguzi uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na vurugu, mashambulizi na uharibifu wa mali.

Post a Comment