Mchungaji,Mary Nnko kutoka kanisa la KKKT Dayosisi ya Morogoro akitoa mada ya Ukatili wa Kijinsia kwa wananchi wa Kijiji cha Kwamhuza Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero,Morogoro
Wananchi wa Kijiji cha Kwamhuza,Kata ya Dakawa,Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro wakifuatilia mada ya Ukatili wa Kijinsia.Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Imani za kishirikina, vitisho na changamoto za kiuchumi zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Kijiji cha Kwamhuza, Kata ya Dakawa, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Hayo yameelezwa katika mkutano wa kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, kupitia mradi wa Msichana Mwenye Malengo Endelevu (Girls With a Purpose – GWAP), unaofadhiliwa na taasisi ya Felm kutoka Finland.
Akizungumza katika mkutano huo, Magreth Pantaleo amesema baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinafanywa kwa malengo maalumu, huku akieleza kuwa baadhi ya wahusika hutumia vitisho vinavyohusishwa na imani za kishirikina ili kuwazuia wahanga na familia zao kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Amesema hali hiyo inawafanya baadhi ya wazazi na walezi kuogopa kuripoti matukio ya ukatili, hasa yanapowahusisha watoto, kutokana na hofu ya vitisho vinavyotolewa na watuhumiwa.
Aidha, amesema changamoto za kiuchumi zinachangia baadhi ya familia kushindwa kuchukua hatua baada ya kutokea kwa matukio hayo, pale zinapopokea fedha kutoka kwa watuhumiwa na kuamua kumaliza kesi kifamilia badala ya kufuata taratibu za kisheria.
Ameeleza kuwa hali hiyo inaweza kuwaacha wahanga bila kupata haki na msaada unaostahili, huku akihimiza jamii kuacha kuficha matukio ya ukatili na badala yake kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika.
Katibu wa Idara ya Wanawake na Watoto wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Mchungaji Dkt. Rhoda Chamshama, amesema hakuna dini inayopaswa kuhalalisha ukatili wa kijinsia, hivyo ni muhimu kwa jamii kuungana katika kupinga na kutokomeza vitendo hivyo.
“Ukatili wa kijinsia haukubaliki kwa dini zote. Tuhakikishe tunapambana kutokomeza ukatili wa kijinsia katika makundi yote. Ukatili unaweza kumpata mtu yeyote bila kuangalia umri wala dini yake,” amesema Mchungaji Dkt. Rhoda.
Amesema kanisa linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Serikali, kutoa elimu kwa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia, namna ya kuutambua na hatua zinazopaswa kuchukuliwa pale tukio linapotokea.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Pelice Lumambo, amesema changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya wananchi kushindwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia, hali inayoweza kuwapa nafasi watendaji kuendelea na vitendo hivyo.
Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote wanaobainika kutenda ukatili.
“Toeni taarifa kwa mamlaka husika ili wote wanaotenda vitendo vya ukatili wa kijinsia wachukuliwe hatua za kisheria, ili tufikie lengo la kutokomeza vitendo hivyo ndani ya wilaya. Ukatili sasa basi,” amesema Lumambo.
Naye Afisa wa Dawati la Jinsia katika Kituo cha Polisi Dakawa, Mwajuma Mkojola, amesema Jeshi la Polisi ni sehemu salama kwa waathirika na watu wenye taarifa kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia, akiwahimiza wananchi kujitokeza kutoa taarifa huku usiri wa watoa taarifa ukizingatiwa.
Mkojola amesema wanaume pia hukumbana na ukatili katika jamii, lakini baadhi yao hushindwa kutoa taarifa kutokana na aibu na hofu, hali inayowafanya kuendelea kuteseka katika mahusiano na ndoa zao.
Amesisitiza kuwa ukatili unapomtokea mtu yeyote, bila kujali jinsia yake, ni muhimu kutoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia malengo ya mradi huo, Mratibu wa GWAP ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Mipango na Maendeleo wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Yona Kitua, amesema kanisa linalenga kujenga jamii yenye amani, utulivu na mazingira yanayowezesha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo bila kukumbwa na vitendo vya ukatili.
Kitua amewahimiza wanajamii kuimarisha mahusiano ya kifamilia na kulinda ustawi wa ndoa, huku akisisitiza umuhimu wa malezi bora na kutatua changamoto za kifamilia kwa njia zinazozingatia usalama na haki za kila mmoja.
Amesema mradi wa Msichana Mwenye Malengo Endelevu (Girls With a Purpose – GWAP) unalenga kupambana na ukatili wa kijinsia, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni, pamoja na kuwawezesha wasichana waliokatiza masomo kurejea shuleni ili waendelee na elimu na kutimiza ndoto zao.
Ameongeza kuwa kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu na kutimiza malengo yake ni hatua muhimu katika kujenga jamii yenye familia imara, malezi bora, amani na maendeleo endelevu.
Kupitia mradi huo, KKKT Dayosisi ya Morogoro inaendelea kuhamasisha ushirikiano kati ya familia, viongozi wa jamii, Serikali na wadau wengine katika kuzuia ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wahanga wanapata msaada na haki zinazostahili.