VIJANA WAKUMBANA NA VIKWAZO BIASHARA ZA MIPAKANI

Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Vijana wanaojihusisha na biashara za mazao ya kilimo katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani wamesema ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu taratibu za biashara na tozo unawaongezea gharama, hali inayoweza kupunguza faida na kuwakatisha tamaa ya kutumia fursa zilizopo.
Wamesema licha ya kuwepo kwa mifumo inayolenga kurahisisha biashara ndogo za mipakani, baadhi ya vijana hawafahamu masharti ya kuitumia, huku wakikabiliwa na changamoto za kupata maelekezo yanayoeleweka kuhusu taratibu za kuvusha bidhaa.

Ofisa programu wa Vijana, Jinsia na Maendeleo ya Ujasiriamali wa AGRA Tanzania, Donald Mezambwa, alisema baadhi ya vijana wamekuwa wakipata changamoto hizo kutokana na kutokujua taratibu zinazopaswa kufuatwa wanapofanya biashara za mipakani.

Akizungumza leo Oktoba 23,2026 katika mdahalo wa kujadili vikwazo vinavyozuia vijana kushiriki kikamilifu katika biashara na uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, Mezambwa amesema ukosefu wa taarifa sahihi unaweza kusababisha wafanyabiashara kulipa gharama zaidi au kupata usumbufu wanapovusha bidhaa.

Amesema katika mijadala iliyofanyika Arusha, vijana kutoka maeneo ya Namanga na Sirari walieleza changamoto walizokutana nazo katika biashara za mipakani, ikiwamo kutokuelewa vizuri taratibu na baadhi ya tozo wanazokutana nazo.

“Unajikuta bora ungelipa kwa usahihi kama ungepata taarifa kuliko kulipa mara mbili au mara tatu zaidi kwa sababu hukuwa na taarifa sahihi,” amesema Mezambwa.

Amesema kuna haja ya Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu na taarifa zinazoeleweka kuhusu taratibu za biashara ili waweze kutumia fursa zilizopo badala ya kuingia kwenye gharama zinazoweza kuepukika.

Mezambwa alitolea mfano utaratibu wa biashara ndogo za mipakani unaojulikana kama Simplified Trade Regime (STR), akisema unaweza kuwa fursa kwa vijana wanaotaka kufanya biashara ya bidhaa zinazovushwa kwenda nchi jirani.

Amesema kwa mujibu wa maelezo yake, utaratibu huo unaruhusu bidhaa zenye thamani isiyozidi Sh milioni mbili kuvushwa bila kulipa kodi zinazohusika, iwapo masharti ya utaratibu huo yametimizwa.
Hata hivyo, amesema vijana wengi wanahitaji kufahamu taratibu na masharti hayo ili waweze kunufaika na fursa hiyo bila kukumbana na changamoto zinazotokana na kutokuwa na taarifa za kutosha.

Amesema Tanzania inapakana na nchi nyingi ambazo zinaweza kuwa masoko ya mazao ya chakula, hivyo kuwawezesha vijana kushiriki katika biashara hizo kunaweza kuongeza fursa za kipato na ajira.

“Wito wetu ni kuhakikisha kwamba Serikali inaangalia namna gani hawa vijana wanapata taarifa sahihi kuhusu nini kifanyike ili waweze kutumia fursa hizi,” amesema.

Ajira kupitia biashara ya kilimo

Mezambwa amesema changamoto za biashara za mipakani ni sehemu ya vikwazo vinavyoathiri ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo kwa ujumla, hali iliyochochea AGRA na wadau wengine kuandaa mdahalo wa kujadili namna ya kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Amesema shirika hilo linatekeleza mradi wa Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture (YEFA), unaofadhiliwa na Mastercard Foundation kwa kipindi cha miaka mitano, kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia kilimo na mifumo ya chakula.
Licha ya hayo ameeleza mradi huo unatumia majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi kutambua changamoto zinazowakabili vijana na kutafuta suluhisho zinazoweza kuboresha mazingira ya biashara.
Kwa mujibu wa Mezambwa, mwaka uliopita majadiliano hayo yalifanyika katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Arusha na Mwanza, huku mwaka huu yakifanyika Mbeya na Arusha.

Amesema baada ya kubaini kuwa changamoto hazihusu biashara za mipakani pekee, wadau waliamua kupanua majadiliano ili kujumuisha vikwazo vingine vinavyowazuia vijana kuingia kwenye biashara za kilimo.
Ameongeza kuwa mkutano huo ulipangwa kuwa wa siku mbili, ambapo siku ya kwanza ililenga kujadili changamoto za vijana, huku siku ya pili ikipangwa kuwakutanisha vijana na wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge zinazohusika na kilimo, viwanda na biashara, maendeleo ya jamii na vijana, pamoja na bajeti.

Amesema lengo la kukutana na kamati hizo ni kuhakikisha changamoto za vijana zinafika kwa watunga maamuzi ili hatua za kisera na kisheria zinazohitajika ziweze kuzingatiwa.

Serikali yaweka mikakati ya kuwawezesha vijana

Kwa upande wake, Clephine Josephat, Msimamizi wa Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) katika Wizara ya Kilimo, alisema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika uzalishaji na biashara za kilimo.

Amesema kilimo kina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania na kina fursa nyingi za ajira katika mnyororo wa thamani, kuanzia uzalishaji mashambani hadi biashara ya mazao na uchakataji.

Josephat amesema Serikali inaendelea kupanua utekelezaji wa BBT katika halmashauri mbalimbali, pamoja na kuweka mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ardhi, mitaji, huduma za ugani na masoko.

Amesema katika mwaka wa fedha husika, Sh bilioni sita zimetengwa kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) kwa ajili ya mikopo inayolenga uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za ugani na kutafuta masoko ya mazao ndani na nje ya nchi ili kuongeza tija na kuifanya sekta hiyo kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana.

Kwa mujibu wa Josephat, BBT inalenga kuchangia upatikanaji wa ajira milioni 1.6 ifikapo mwaka 2030, huku ikilenga kuwezesha ekari 340,000 kuwa kwenye uzalishaji na kupanua programu hiyo hadi vijiji vyote 12,000 vya Tanzania Bara.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau kama AGRA ni muhimu katika kuhakikisha mawazo ya vijana yanafika kwa watunga maamuzi na kuzingatiwa katika mipango ya maendeleo ya kilimo.

Vijana wataka taarifa zinazofikika

Naye Charles Constantine Masasi, Mkurugenzi wa Tavia Agribusiness Company Limited, alisema ukosefu wa taarifa kwa wakati ni miongoni mwa changamoto zinazowafanya vijana washindwe kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na wadau wa sekta ya kilimo.
Masasi, ambaye alisema kampuni yake inajihusisha na uzalishaji wa mbegu na inaelekeza uwekezaji pia kwenye mboga mboga na matunda, alisema vijana hawawezi kuchangamkia fursa ambazo hawazifahamu.

Amesema kupitia programu ya BBT, kampuni yake iliweza kubaini pengo katika upatikanaji wa mbegu na kuhamasisha vijana wengine kushiriki katika uzalishaji ili kusaidia wakulima.

Kwa mujibu wa Masasi, juhudi hizo ziliiwezesha kampuni kupata mkataba wa Serikali mwaka 2024 kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, ikiwamo gharama za pembejeo na masharti ya mikopo ambayo yanaweza kuathiri uwezo wa vijana kuanzisha na kukuza biashara zao.
Amesema ni muhimu taarifa kuhusu mikopo, ardhi na fursa nyingine za kilimo zitolewe kwa uwazi na kwa njia zinazoweza kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.

Anasisitiza kuwa uwepo wa fursa pekee hautoshi bila mifumo inayowawezesha vijana kuzifahamu, kuzipata na kuzitumia kwa manufaa ya biashara zao.

Kwa washiriki wa mdahalo huo, kuboresha upatikanaji wa taarifa za biashara za mipakani ni hatua mojawapo inayoweza kusaidia kupunguza vikwazo vya kibiashara, kupanua masoko ya mazao na kuongeza ushiriki wa vijana katika mifumo ya chakula.




Post a Comment