SERIKALI YAKOMESHA MIGODI KUAGIZA HUDUMA NJE YA NCHI,YAOKOA SH BILIONI 5.1

 

SERIKALI ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha rasilimali za madini nchini zinawanufaisha Watanzania moja kwa moja kwa kugeuza maeneo ya migodi kuwa vitovu vya viwanda na biashara.

Akizungumza katika ziara yake kwenye Eneo Maalumu la Kiuchumi la Buzwagi (BSEZ) wilayani Kahama hivi karibuni, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kuwa serikali imedhamiria kukomesha utaratibu wa migodi kuagiza huduma na bidhaa kutoka nje ya nchi, jambo linalopoteza takribani Sh bilioni 5.1 kila mwaka.

Mkakati huo wa serikali unahusisha kugeuza eneo la Mgodi wa Barrick Buzwagi, lenye ukubwa wa hekta 1,333, kuwa eneo maalumu la viwanda baada ya shughuli za uchimbaji kusitishwa. Badala ya eneo hilo kubaki gofu, serikali imeweka miundombinu ya kisasa kuvutia wawekezaji.

"Malengo yetu ni kuifanya Kahama kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa migodi ya ndani na hata nje ya nchi. Tunataka fedha zinazotoka nje ya nchi zibaki nchini Tanzania," alisema Mavunde.

Waziri Mavunde amesisitiza kuwa serikali imeweka mazingira rafiki na kipaumbele kwa wawekezaji wazawa. Alibainisha kuwa kisheria, kuna huduma na bidhaa zaidi ya 20 ambazo wageni hawaruhusiwi kuwekeza, hivyo kuwapa uwanja mpana Watanzania kuchangamkia fursa hizo.

Uwekezaji huu unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 5,000 zilizokuwepo awali wakati wa uchimbaji, huku kampuni ya Nickel ikiwa tayari imeweka mtambo wa uchenjuaji wa dhahabu utakaosaidia wachimbaji wadogo wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amethibitisha kuwa tayari wawekezaji 15 wameonyesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo. Alitaja vivutio kama uwepo wa barabara bora, hoteli za kisasa, kiwanja cha ndege, na reli ya kisasa (SGR) itakayounganishwa kutoka Bandari Kavu ya Isaka hadi ndani ya eneo la uwekezaji.

"Mikakati imewekwa kuunganisha reli kutoka Isaka hadi ndani ya eneo hili ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa hadi asilimia 50," alisema Mhita, huku akiongeza kuwa kampuni kubwa kama Dangote (GSM) na TRC tayari zimeanza ujenzi wa vituo vya mizigo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri, ameeleza kuwa eneo la Buzwagi lina faida ya kijiografia kutokana na ukaribu wake na masoko ya nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, DRC, na Sudan Kusini.

Mbunge wa Kahama, Benjamin Ngayiwa, na mwenzake wa Msalala, William Magangila, wamepongeza hatua hiyo wakisema italeta neema kwa vijana na wachimbaji wadogo ambao sasa watapata vifaa vya utambuzi wa madini na zana za kazi kwa bei nafuu kutokana na kuzalishwa ndani ya nchi.

Nao wakazi wa Kahama, Hamza Hassan na Salome Gabriel, wameonyesha matumaini makubwa, wakisema uwekezaji huo utachochea biashara ndogondogo kama za 'mama lishe' na kuwawezesha kumudu gharama za maisha na masomo kwa watoto wao.

Post a Comment