SERIKALI YAPELEKA 'MAMA SAMIA LEGAL AID' WILAYANI KUIMARISHA AMANI

 SERIKALI ya Awamu ya Sita imetangaza mkakati mpya wa kuimarisha haki na amani nchini kwa kuipanua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia hadi ngazi ya wilaya nchi nzima.

 Hatua hiyo iliyotangazwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, inalenga kuondoa kero na migogoro inayowakabili wananchi katika maeneo yao, hususan wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za kisheria.

Akiwa mkoani Morogoro, Dk. Homera amebainisha kuwa wizara imejipanga kuwafuata wananchi walipo ili kuwasogezea huduma hizo muhimu.

 Kampeni hii imejikita katika kutoa elimu na utatuzi wa changamoto za kisheria kwenye masuala mtambuka yakiwemo ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, na usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala. Lengo kuu ni kuhakikisha misingi ya haki za binadamu na utawala bora inaimarika kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa.

Uamuzi wa kupeleka huduma hizi wilayani unakuja baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wananchi milioni 40 walifikiwa na kunufaika na kampeni hiyo. 

Kupitia usikilizaji wa mamilioni ya kero za kisheria, serikali imeweza kurejesha utulivu na mshikamano katika jamii nyingi zilizokuwa zimegubikwa na migogoro ya muda mrefu ya ndoa na ardhi.

Amani na Uchumi.

Uamuzi wa kumfuata mwananchi alipo unatajwa kuwa ni "Habari Njema" kwani msaada wa kisheria una uhusiano wa moja kwa moja na amani ya nchi. Wananchi wanapopata haki zao, migogoro hupungua, jambo linalopelekea,Kuimarika kwa utulivu na mshikamano wa kitaifa.

"Jukumu letu ni kuwafuata wananchi ili wanufaike na serikali yao. Tunataka kuondoa changamoto zinazowakabili ili kila mmoja ashiriki katika ujenzi wa taifa akiwa na amani moyoni," amesisitiza Dk. Homera.

Ufikishaji wa huduma hizi ngazi ya chini una tija kubwa katika kuimarisha amani na utulivu wa taifa. Wananchi wanapopata haki zao, hupata utulivu wa moyo unaowawezesha kujikita katika shughuli za uzalishaji mali na kuongeza kipato chao.

 Hivyo, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia si tu chombo cha kutoa haki, bali ni injini ya kuleta utengamano wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake na watoto. 

Post a Comment