WAKATI WACHOCHEZI WA MTANDAONI WAKITABIRI ANGUKO, DUNIA YAWEKEZA TANZANIA


   WAKATI  wanaojidai wanaharakati wa mtandaoni  wakipiga ramli kuwa Tanzania imekwisha, dunia imeendelea kuwaumbua kwa vitendo. 

Katika mwendelezo wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, kundi kubwa la wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Ujerumani (German Agribusiness Alliance) limethibitisha rasmi kuja kuwekeza nchini.

Hatua hiyo imekuja kufuatia diplomasia ya uchumi iliyofanywa jijini Berlin, Ujerumani ambapo Tanzania imeonekana kuwa nchi yenye utulivu wa kipekee, sifa ambayo wawekezaji duniani kote wanaitafuta kwa udi na uvumba.

Akiongoza msafara wa Tanzania pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa la Chakula na Kilimo (GFFA) nchini Ujerumani, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewaalika wawekezaji hao kushiriki Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nane Nane mwezi Agosti 2026 na baada ya mazungumzo walikubali.

Katia mkutano huo Ujumbe wa Tanzania uliwasilisha fursa kemkem katika masuala ya uzalishaji wa mbegu za mafuta, ngano, na soya. Pia Tanzania ilielezea fursa katika masuala ya uchakataji wa mazao kama kakao, kahawa, na korosho. 

Fursa nyingine zipo katika miundombinu ya uhifadhi na usafirishaji wa mazao ya bustani (Horticulture) na teknolojia ikihusisha zana za kisasa na mifumo ya umwagiliaji.

 Dunia Inatuelewa

"Kama walisema tumekwisha, sasa wao ndio wamekwisha. Tanzania inasonga mbele kwa sababu nchi yenye utulivu ndiyo inayovutia uwekezaji," kilieleza chanzo kimoja ndani ya wizara kikisherehekea mapokezi makubwa ya Tanzania nchini Ujerumani.

Mwenyekiti wa German Agribusiness Alliance, Frank Karl Nordmann, amethibitisha kuwa wataingia nchini kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026, siyo tu kuonesha bidhaa zao, bali kubadilishana teknolojia na uzoefu katika mnyororo wa thamani wa kilimo na mifugo.

Mapinduzi ya Kidijitali na Mifugo

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kupanua mifumo ya kidijitali katika kilimo. Lengo ni kuongeza uzalishaji wa mazao na mifugo kufikia viwango vya juu ambavyo havijawahi kushuhudiwa, ili kuifanya Tanzania kuwa "ghala la chakula" la Afrika na dunia.

Kwanini Mataifa Makubwa Yanakuja Tanzania Sasa?

Wataalamu wa masuala ya siasa na uchumi wamebainisha sababu tatu kuu zinazowafanya waje . Nazo ni utulivu wa kisiasa, uaminifu wa uongozi na uthubutu. 

Katika suala la utulivu wa kisiasa wanasema tofauti na majirani au mataifa yanayokumbwa na migogoro, Tanzania imebaki kuwa kisiwa cha amani.

Aidha kwenye uaminifu wa kiongozi,Rais Samia Suluhu Hassan amejenga daraja la uaminifu kati ya serikali na wawekezaji wa nje huku uthubutu wa ujenzi wa Miradi ya kimkakati kama ya umeme na ujenzi wa miundombinu inawapa uhakika wawekezaji kuwa nchi iko tayari kwa viwanda.

Pamoja na kelele wanazopiga wachochezi Tanzania haijawahi kuwa imara kama ilivyo sasa. Kutoka tuzo za utalii duniani hadi kuvutia matajiri wa Ujerumani kwenye kilimo, huu ni ushahidi kuwa nchi inapaa. Wale wanaosubiri nchi ianguke, wataendelea kusubiri huku maendeleo yakipita mlangoni kwao.  

Post a Comment